VIFUNGASHIO VYA PLASTIKI (TUBINGS NA WRAPPINGS) VISIVYOKIDHDI VIWANGO VYAPIGWA MARUFUKU


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Mhandisi Dkt.Samuel Gwamaka amepiga marufuku matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za NEMC Makao Makuu Mikochenijijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa vifungashio vya plastiki vinavyotumika kufungashia bidhaa kama karanga, ubuyu, barafu na chupa za maji ambavyo havina vibali kutoka Shirika la viwango Tanzania (TBS). Pia katika masoko yetu hali inaonyesha kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivigine kama vibebeo.

“Uwepo wa vifungashio hivi sokoni unaenda kinyume na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki, ya mwaka 2019.Madhumuni ya Kanuni hizi nikupiga marufuku uingizaji nchini, usafirishaji nje ya nchi, uzalishaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki; kulinda afya ya binadamu na wanyama pamoja na mazingira dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya mifuko ya plastiki; na kutoa motisha kwa ajili ya kuhamasisha uzalishaji na uingizaji nchini wa mifuko mbadala ambayo inaoza” amesema Dkt. Gwamaka.

Aidha, ameeleza kuwa kuna athari nyingi zinazojitokeza kutokana na matumizi ya mifuko hiyo hivyo ni bora Wananchi kutumia fursa zilizopo kuzalisha mifuko mbadala ambayo haina athari kwa kizazi kilichopo na kijacho.

“Kwa mfano, imebainika kuwa vifungashio hivi visivyokidhi viwango vina athari kwa watoto pale wanapotafuna vifungashio hivyo na kumeza chembechembe ndogo za plastiki. Hali kadhalika, baadhi ya wafungashaji wa bidhaa wamekuwa wakipuliza vifungashio hivyo ili kupata urahisi wa kuweka bidhaa na hivyo kuhatarisha afya ya walaji kunakoweza kupelekea kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza” Dkt. Gwamaka alisema.

Aliendelea kueleza kuwa Kanuni ya katazo la mifuko ya plastiki, sehemu 4, inatoa mwongozo wa matumizi ya vifungashio vya plastiki yanayoruhusiwakuwa vitumike pale tu itakapobainika kuwa bidhaa husika inaulazima wa kutumia vifungashio vya plastiki.

Kwa mujibu wa sehemu ya 3 ya Kanuni ya Katazo la Mifuko ya Plastiki,inatafsiri ulazima huo kuwa ni, Kuhifadhi ubora au kuzuia uharibifu wa bidhaa, na vifungashio viwe ambavyo vitakuwa na lakiri au alama inayotambulisha kikamilifu bidhaa iliyofungashwa kabla ya kuingia sokoni.

“Kwa mujibu wa Kanuni ya Katazo la mifuko ya plastiki sehemu ya 6, viwanda vyotevinavyotumia vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango vilivyowekwa kama vinavyotumika kufungashia chupa za vinjwaji na vitu vingine ni kosa kwa mujibu wa sheria.” Alisema Dkt. Gwamaka.

Pia aliendelea kueleza kuwa watakao kaidi agizo hili hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kutozwa faini na kupelekwa mahakamani. NEMC imefanya kazi ya ziada kutoa elimu kwa wazalishaji, wasambazaji na watumiaji, hivyo sasa hivi ni muda wa kutekeleza tu sheria.

“Tunaomba Wananchi kutoa taarifa NEMC pindi watakapo baini kuna wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa vifungashio vya plastiki vilivyokatazwa ili kuwakamata hao wahalifu. Mwananchi akitoa taarifa kuisaidia Serikali itakuwa ni siri na atapewa asante yake, hii ni kuweza kufanikisha zoezi hilo kwa ufasaha" amesema Dkt. Gwamaka.

Jitihada mbalimbali zilishachukuliwa hapo awali ili kuhakikisha sheria inatekelezwa na changamoto zinatatuliwa. Jitihada hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuandaa rasimu ya viwango vya vifungashio kwa kuwashirikisha wadau pia kufanya mikutano na wadau wa sekta ya uzalishaji wa vifungashio ili kuwaelimisha jinsi ya kutekeleza sheria.

Pia Dkt. Gwamaka amewataka wadau wote kushirikiana katika kutekeleza sheria hii ili kuhifadhi na kulinda mazingira yetu.