​MAKAMU WA RAIS AIPONGEZA NEMC KWA UTOAJI ELIMU YA UDHIBITI WA TAKA ZA PLASTIKI – AITAKA IONGEZE KASI ZAIDI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa juhudi zake katika kutoa elimu kuhusu udhibiti wa taka za plastiki, na kulitaka Baraza kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Mhe. Dkt. Mpango ametoa pongezi hizo leo, tarehe 5 Juni 2025, alipotembelea banda la NEMC katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

“Nawapongeza kwa juhudi mnazozifanya katika kutoa elimu kuhusu udhibiti wa taka za plastiki. Ni muhimu kuongeza kasi zaidi ili wananchi waelewe namna ya kupunguza, kutumia tena na kurejeleza taka hizi kwa ajili ya kuzalisha bidhaa nyingine,” alisema Mhe. Dkt. Mpango.

Aidha, Makamu wa Rais alieleza kuwa kuna haja ya kuongeza msukumo katika maboresho ya Sheria ili kulifanya Baraza kuwa Mamlaka kamili ya Usimamizi wa Mazingira nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipokea maagizo ya Makamu wa Rais na kusema wasilisho lililotolewa na Meneja wa Kanda ya Kati Bw. Novatus Mushi ni sehemu ya Utekelezaji wa mkakati wa udhibiti wa taka za plastiki na kuwa Baraza linaendelea kusimamia Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira kwa kuhakikisha shughuli za Uhifadhi wa Mazingira zinakuwa endelevu.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2025 yameambatana na maonesho yaliyofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 5 Juni, Pia yamebebwa na kauli mbiu isemayo: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa; Dhibiti Matumizi ya Plastiki.”