Usajili wa Wataalamu

USAJILI NA UTENDAJI WA WATAALAM ELEKEZI WA MAZINGIRA

Sehemu ya 83 (1) ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imeweka bayana kwamba Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) inapaswa kufanywa na Mtaalam Elekezi wa Mazingira aliyesajiliwa na Baraza.Usajili huo hufanyika kwa kuzingatia Kanuni ya Mazingira (Usajili na Utendaji wa Wataalam Elekezi wa Mazingira) ya mwaka 2021 ambayo inatoa jukumu hilo na mengine kwa Msajili wa Wataalam wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira.

Pamoja na kusajili Wataalam Elekezi, Baraza linajukumu la kusimamia mwenendo wa Wataalam hao na kuchukua hatua za kinadhamu kwa mujibu wa sheria pale ambapo Baraza litajiridhisha kwamba kosa limefanyika.Hatua hizo ni pamoja na kufungia, kumuamuru alipe faini au fidia, kutoa onyo na hata kufuta usajili wake.

Aidha, Kanuni ya 24.-(1) inakataza Mshauri Elekezi wa Mazingira kufanya TAM bila cheti cha utekelezaji ambacho kinaisha baada ya miaka mitatu. Wataalam Elekezi wenye cheti cha utendaji na wasio na deni lolote Baraza, na ambao majina yao yatatangazwa katika tovuti ya Baraza ndio wanastahili kufanya TAM na Ukaguzi wa mazingira.

Wenye nia au lengo la kufanya TAM lazima watatuma maombi kwa Baraza kwa kujaza fomu husika na kulipia kiwango cha pesa kilicho ainishwa.Maombi yote yanafanyika mtandaoni kupitia eia.nemc.or.tz.

Muombaji anaweza kuwa binafsi au kampuni ya Wataalam Elekezi.Baraza linapokea maombi ya usajili na utendaji wa TAM na Ukaguzi wa mazingira kipindi chote cha mwaka.Hii ni pamoja na maombi kutoka kwa raia wa kigeni ambao wanaweza kutuma maombi ya kupewa leseni ya utendaji kwa mradi maalumu.