Kanda ya Magharibi

<>

Utangulizi

Ofisi za Kanda zilianzishwa ili kuhakikisha Dhima ya Baraza inatekelezeka kwa ufanisi zaidi hususani katika kutimiza majukumu yake kikanda na kutoa huduma karibu zaidi na jamii. Ofisi ya Kanda ya Magharibi ni mojawapo ya ofisi 9 za kanda zilizowekwa kimkakati katika maeneo mbalimbali nchini. Kanda hii ilianza rasmi kutimiza majukumu yake mnamo Mwezi Julai, 2019. Kanda inahudumia Mikoa 4 (Kagera, Kigoma, Katavi na Rukwa) na ofisi zake ziko katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji katika anuani ifuatayo.

NEMC - Kanda ya Magharibi,

Ghorofa ya 1 NSSF Mafao House,

Mtaa wa Mnarani,

S. L. P 974,

Kigoma/Ujiji, Tanzania,

Simu: +255 738 037307;

barua pepe: nemckigoma@nemc.or.tz

Tovuti: www.nemc.or.tz

Eneo la kanda

Kanda ina eneo la kilomita za mraba zipatazo 161,954.309 ikiwa ni sawa na takriban asilimia 17 ya eneo lote la Nchi. Kanda hii inahudumia Mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi na Rukwa inayojumuisha Wilaya 19 na Halmashauri 25 kama ifuatavyo;

1.Mkoa wa Kagera unaojumuisha Wilaya 7 na Halmashauri 8. Wilaya zilizopo katika mkoa huu ni Bukoba, Karagwe, Biharamulo, Kyerwa, Muleba, Ngara na Missenyi. Halmashauri zilizopo katika mkoa huu ni Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi na Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa.

2.Mkoa wa Kigoma unaojumuisha Wilaya 6 na Halmashauri 8. Wilaya zilizopo katika mkoa huu ni Kigoma, Kasulu, Buhigwe, Kibondo, Kakonko na Uvinza. Halmashauri zilizopo katika mkoa huu ni Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.

3.Mkoa wa Katavi wenye Wilaya 3 na Halmashauri 5; wilaya zilizopo katika mkoa huu ni Mpanda, Mlele na Tanganyika. Halmashauri zilizopo katika mkoa huu ni Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo zilizopo katika Wilaya ya Mpanda, Halmashauri za Wilaya ya Mlele na Mpimbwe zilizopo katika Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika iliyopo katika Wilaya ya Tanganyika.4.Mkoa wa Rukwa wenye Wilaya 3 na Halmashauri 4. Wilaya zilizopo katika mkoa huu ni Sumbawanga, Kalambo na Nkasi. Halmashauri zilizopo katika mkoa huu niHalmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Mipaka ya kanda

Kanda ya Magharibi inapakana na Nchi 4: Upande wa Kaskazini iko nchi ya Uganda; Nchi za Rwanda, Burundi na DR Congo ziko upande wa Magharibi na Zambia upande wa Kusini. Kanda hii pia inaungana na Mikoa 3: Mbeya katika Upande wa Kusini; Tabora na Geita kwa upande wa Mashariki.

Kanda ya Magharibi pia imebarikiwa kuwa Maeneo na Mifumi Ikolojia nyeti yenye umuhimu kitaifa na kimataifa. Maeneo haya pamoja na Maziwa makuu 3 (Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa) Mito mikubwa miwili (Mto Kagera na Mto Malagarasi) Hifadhi 4 za Taifa (Burigi – Chatto, Mahale, Gombe na Katavi) Hifadhi hai 1 (Gombe Masito Ugalla) Bonde oevu la Malagarasi – Moyowosi vile vile Misitu mbalimbali ya Hifadhi.

Majukumu

NEMC Kanda ya Magharibi ilianzishwa kwa madhumuni ya kutelekeza majukumu na huduma za Baraza karibu na jamii za mikoa iliyo ndani ya kanda kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu. Majukumu miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na;

i.Kuratibu na kuunganisha vyombo mbalimbali vya Serikali katika masuala yanayohusiana na Usimamizi na Uhifadhi wa mazingira kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 na Kanuni zake;

ii.Kuongeza uelewa kwa umma kuhusu masuala ya Usimamizi wa Mazingira;

iii.Kuhakikisha kunakuwa na Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni zake katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

iv.Kuhakikisha miradi ya maendeleo kabla ya kutekelezwa inafanyika Tathmini ya Athari kwa Mazingira au kwa iliyopo inafanyiwa Ukaguzi wa Awali wa Mazingira, ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya miradi hiyo ili kupata Cheti cha Mazingira;

v.Kushughulikia Malalamiko, Matukio na Maoni mbalimbali ya Mazingira yanayowasilishwa Ofisini;

vi.Kutoa miongozo kwa jamii kuhusiana na masuala mbalimbali ya Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira;

vii.Kusimamia utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayohusu Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira na Mali asili.

viii.Kuendesha na kuratibu tafiti mbalimbali za usimamizi wa mazingira.