Utangulizi

UTANGULIZI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilianzishwa kwa Sheria ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira Na. 19 ya mwaka 1983 kama chombo cha kuishauri serikali juu ya masuala ya utunzaji endelevu wa mazingira. Baraza lilianza kazi rasmi mwaka 1986. Sheria Na. 19 ya mwaka 1983 ilifutwa mwaka 2004 na Sheria ya Usimammizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 (Sura 191) ambayo ilianzisha Baraza kwa mara nyingine. Sheria hii mpya ililipa Baraza nguvu ya kisheria ya kusimamia hifadhi ya Mazingira nchini

Tangu kuanzishwa kwake Baraza limekuwa likisimamia na kutoa ushauri kwa serikali kuhusu suala zima la hifadhi ya mazingira nchini. Kwa mujibu wa kifungu cha 17cha Sheria hiyo madhumunina sababuza kuanzisha Baraza hili nikuratibu utekelezaji wa sera na sheria ya mazingira katika nyanja kuu nne:- Kutekeleza shughuli za uzingatiaji na usimamizi (enforcement and compliance) wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira; Kusimamia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) (Kuratibu, kufanya mapitio ya ripoti zaTAM kutoka kwa wenye miradi na kufuatilia utekelezaji wake); Kuwezesha ushiriki wa umma katika kufanya uamuzi unaohusu mazingira na Kusimamia kwa ujumla na kuratibu masuala yote yanayohusu mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Sheria nyingine zozote zilizoandikwa.

Aidha, kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, inatoa mchanganuo mpana wa majukumu ya Baraza kama ifuatavyo:-Kufanya uhakiki wa mazingira (Environmental Audit), Kufanya tathmini ambazo zitasaidia katika kuhifadhi na kusimamia, Kufanya utafiti na kuratibu utafiti wa mazingira, kuchunguza, kutathmini na kukusanya taarifa na matokeo ya utafitina kuzisambaza kwa wadau, Kufanya mapitio na kutoa mapendekezo ili kuwezesha kupitishwa kwa taarifa/ripoti za TAM), Kuainisha miradi au programu zinazohitaji kufanyiwa ukaguzi na ufuatiliaji (Audit and Monitoring)

Kuhimiza na kuhakikisha usimamizi na uzingatiaji wa viwango vya taifa katika utekelezaji wa sheria, Kuanzisha hatua madhubuti zenye lengo la kulinda na kudhibiti ajali zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira na kubuni njia za kurekebisha maeneo ambayo yamepata uharibifu, Kutekeleza programu zenye lengo la kutoa elimu ya mazingira na kukuza weledi kwa kushirikiana na taasisi na sekta za wizara mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha usimamizi madhubuti na ushiriki wa jamiikatika shughuli za kuhifadhi mazingira, Kuchapisha na kusambaza miongozo mbali mbali ya usimamizi wa mazingira inayolenga udhibiti wa uharibifu wa mazingira, Kutoa ushauri wa kitaalam na kusaidia taasisi na asasi mbali mbali zinazoshughulika na usimamizi wa maliasili na mazingira, na Kufanya shughuli nyingine zozote kwa maagizo ya Waziri wa Mazingira au kutokana na uhitaji wakati wa utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.