UMUHIMU WA VYANZO VYA MAJI KATIKA KUTUNZA MAZINGIRAMiongoni mwa vivutio vikubwa katika mazingira ni uwepo wa vyanzo vya maji vya aina mbalimbali. Si tu vivutio bali kwa kiasi cha zaidi ya 80% ndio hujenga maisha ya mwanadamu, kwani vyanzo vya maji hutumika katika shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Vyanzo vya maji jumla ya maeneo yote ambayo maji huanzia hapo kabla ya kusafiri Kwenda sehemu nyinginezo. Kwa mfano Mito, Maziwa, Visima, Chemichemi, Mabwawa nk. Kimsingi maji ndio kiini cha uhai wa viumbe hai vyote vilivyopo duniani. Iwe ni Binadamu, Wanyama na Mimea, vyote haviwezi kuishi bila ya uwepo wa maji safi na salama.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaaliwa aina tofauti tofauti za vyanzo vya maji, ikiwemo mito, mabwawa, maziwa, nk. Licha kujaaliwa uko kwa kuwa na aina nyingi za vyanzo vya maji, bado wananchi wake huvitumia vyanzo hivyo kimakosa kwa kutovilinda na kuvitunza na kusababisha baadhi ya vyanzo hivyo kutokuwa endelevu.

Shughuli za kibinaadamu kwa kiasi kikubwa huchangia uharibifu wa mazingira na hivyo kupelekea uchafuzi wa vyanzo hivyo vya maji na kupoteza ule muonekano na matumizi ya awali.Zipo shughuli mbalimbali za kibinaadamu ambazo husababisha uchafuzi wa vyanzo hivyo vya maji, na miongoni mwa hizo ni kukata miti hovyo pembezoni mwa vyanzo vya maji, kutupa taka ngumu karibu na vyanzo vya maji au katikati ya vyanzo vya maji, kwa mfano kutupa chupa za vioo, makopo ya plastiki, na mifuko, pia kupitisha maji taka tiririka toka viwandani kuelekea katika vyanzo hivyo na kusababisha maji katika vyanzo hivyo kuwa na mchanganyiko wa kemikali sumu zitokazo viwandani.

Upo umuhimu mkubwa sana katika kutunza mazingira unaotokana na vyanzo vya maji katika jamii yetu nan chi kwa ujumla, kama vyanzo hivyo vikitunzwa ipasavyo.

Husaidia katika udhibiti wa magonjwa ya mlipuko. Magonjwa kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, na kuhara kwa kiasi kikubwa husababiswa na uchafuzi wa mazingira hususani vyanzo vya maji. Uchafuzi huo husababisha maji kupokea vimelea vya magonjwa na maji hayo yanapotumika na wanadamu vile vimelea vilivyomo katika maji huenda kuathiri afya za wanadamu na kusabisha magonjwa mbalimbaliu.

Umuhimu mwengine ni kukuza mimea na kufanya mazingira yetu kuwa yakijani. Kwa kiasi kikubwa ukijani wa mazingira utokanao na mimea huonesha mvuto mkubwa , na kusaidia kuwepo kwa hewa ya Oxygen kwa wakati wote. Wanadamu na wanyama tunaitaji hewa ya Oxygen ili kuendesha shughuli nyingine za mwili. Sio hivyo tu, wakati mimea hutoa hewa safi ya Oxygen ni kwa wakati huo huo yenyewe hufyonza hewa chafu ya ukaa (Carbon dioxide) hivyo husaidia kupunguza joto na hewa chafu hapa duniani.

Vyanzo vya maji hutumika kama makazi ya baadhi ya viumbe hai. Viumbe kama vile Samaki, Vyura na Ndubwi huishi majini na, kwa kuvitunza vyanzo vyetu vya maji kunafanya viumbe hao waendelee kuwepo na kuzaliana kwa wingi na katika hilo ndipo tutaona umuhimu wa hao viumbe waishio majini katika mzingira yetu. Kwa mfano, Sanaki hutumika kama kitoweo kwa bvinadamu na baadhi ya samki hutumika kama mapambo katika sehemu mbalimbali ikiwemo majumbani na hivyo kufanya mazingira yetu yavutie.

Kwa upande mwengine, vyanzo vya maji husaidia katika kukuza na kuendeleza kilimo kwani husaidia kuhahakiksha kuwa kunakuwa na maji wakati wote kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji. ukiachilia mbali kilimo cha umwagiliaji, pia kwa kukuza mimea vizuri ndio tunapata mvua katika vipindi husika vya majira na hivyo husaidia na wakulima kuwa na uhakika na mvua kwaajili ya mazao yao.

Serikali kupitia Baraza la Taifa la Mazingira linasisitiza umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji katika mazingira yetu kwaajili ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinabaki salama, wananchi wanahimizwa kutotupa taka ya aina yeyote ile katika vyanzo vya maji na badala yake wahakikishe taka zote zinawekwa sehemu husika, lakini pia kupanda miti katika maeneo yote yaliyowazi hususani kando ya vyanzo vya maji ili kujihakikishia usalama wa vyanzo hivyo. Pia serikali kupitia Baraza, inahimiza kuwa shughuli zote za kibinadamu zinazofanyika kando au ndani ya vyanzo vya maji ikiwemo uvuvi na uchimbaji wa madini kuhakiksha kuwa zinafuata sheria na kanuni zilizowekwa kwaajili ya usalama zaidi na kuepuka uchafuzi usio wa msingi kwa vyanzo vyetu vya maji. Kwani, vyanzo vya maji visipokuwa salama, huatarisha maisha ya wanadamu na viumbe hai vingine viishivyo majini.