UHARIBIFU VYANZO VYA MAJI NA ATHARI ZAKE


UHARIBIFU VYANZO VYA MAJI NA ATHARI ZAKE

UTANGULIZI

Nchi yetu imejaliwa kuwa na vyanzo vya maji vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na mito, maziwa, ardhi oevu na maji ya chini ya ardhi. Vyanzo vya maji ni rasilimali muhimu inayochangia maendeleo ya nchi, kwani tunapata maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha nishati ya umeme, maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli mbalimbali za maendeleo nchini. Kutunza vyanzo vya maji ni kujiwekea mazingira mazuri ya kulinda afya ya jamii, kujenga uchumi endelevu wa nchi kwa ujumla.

UHARIBIFU WA VYANZO VYA MAJI NA ATHARI ZAKE
Licha ya kuwepo na Sheria za Usimamizi wa vyanzo vya maji (bahari, maziwa, mito, mabwawa, na chemichemi) kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji kutokana na kuwepo kwa shughuli za binadamu zinazofanyika pasipo kiuzingatia Sheria zinazosimamia mazingira na rasilimali maji. Shughuli hizo ni pamoja na ukataji wa miti kwa ajili ya kujipatia kuni, mkaa au mahitaji ya ujenzi, mifugo, uchimbaji mchanga na madini, na ujenzi usiozingatia taratibu taratibu za mipango miji, kilimo kisicho endelevu. Pia shughuli za uchimbaji mchanga kwenye maeneo ya mito na uchimbaji madini kwenye vyanzo vya maji, kilimo na maogesho ya mifugo katika vyanzo hivyo vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa vyanzo vya maji hususani kuongeza matope kwenye vyanzo vya maji. Vilevile uchepushaji wa maji kutoka katika vyanzo vya maji pasipo kuzingatia sheria na taratabu zilizowekwa na serikali za uchukuaji maji kwenye vyanzo vya maji (wenye vibali vya kuchota maji kuchukua maji zaidi ya viwango vilivyoidhinishwa).

Vilevile, shughuli za binadamu zinachangia mabadiliko ya tabianchi (ongezeko la muda mrefu la joto la wastani la dunia) ambalo hupelekea kubadilika kwa mfumo mzima wa hali ya hewa. Mabadiliko ya Tabianchi ni tatizo linaliokabili dunia katika karne ya ishirini na moja na kutokana na athari zake katika nyanja mbalimbali. Aidha, mabadiliko ya tabia nchi yameathiri kwa kiasi kikubwa vyanzo vya maji na kusababisha vyanzo hivyo kukauka na kupunguza uwezo wake wa kuzalisha maji na kupungua kwa ubora wa maji. Hali hizo zimeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji kwenye maeneo mbalimbali nchini. Mfano mwaka 2021 mwishoni tumeshuhudia upungufu mkubwa wa maji katika bonde la Mto Wami/Ruvu ambalo ni tegemeo kubwa la maji yanayohudumia mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Changamoto hii inatokana na uharibifu uliokithiri wa mazingira katika bonde la mto Ruvu. Uendelevu wa shughuli hizi pasipo kuzingatia Sheria kutaendelea kuathiri vyanzo cha maji halia ambavyo na itapelekea ukosekanaji wa ubora na wingi wa maji.

Athari nyingine zinazojitokeza kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji ni pamoja na ukosekanaji wa ubora na wingi wa maji ambayo ni tegemeo kwa wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kilimo na shughuli nyingine za maendeleo, mlipuko wa magonjwa kutokana na kutokuwa na majisafi na salama, kwani yatakosekana au kuwa machache. Vilevile uchafuzi wa vyanzo vya maji kutokana na matumizi ya viuatilifu vinavyotumika kuua wadudu ya kutunza mimea. Viuatilifu hivyo huingia kwenye maji hayo, hali ambayo inaweza kusababisha ongezeko la magonjwa mengi yasiyotibika, kupungua kwa kina cha maji kwenye mito, kupotea kwa biounuwai na uchafuzi wa maji. Hali hii husababisha kuongezeka kwa gharama ya kuchakata maji ghafi. Aidha maji yaliyochafuliwa huhitaji kiwango kikubwa cha madawa ya kutibu na kusafisha maji kutokana na uchafuzi wa mazingira katika vyanzo vya maji.

JITIHADA ZINAZOTAKIWA KUKABILIANA NA ATHARI KWENYE VYANZO VYA MAJI

Swala la utunzaji wa vyanzo vya maji ni la kila mwanajamii, hii ni kuhakikisha kila mmoja anakuwa balozi mzuri wa kuona namna ya kuvilinda na kuvitunza vyanzo vya maji. Hivyo ni muhimu kila mmoja wetu kushirikiana kikamilifu katika kuhakikisha maeneo ya vyanzo vya maji hayachafuliwi na hayaharibiwi. Katika kutekeleza adhma hiyo, ni muhimu kwa kila taasisi na kila mmoja kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake hasa zinazoelekeza kuhusu uhifadhi wa vyanzo vya maji. Lengo ni kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu.

Aidha taasisi husika zinatakiwa kuendelea kutoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo ya vyanzo vya maji. Kuepuka kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji. Vilevile kutumia mbinu mbadala na endelevu za kilimo. Serikali za mitaa na vijiji kuwa na mipango madhubuti ya kutunza vyanzo vya kwenye maeneo yao kama kushirikiana na Wizara ya Mifugo kuhakikisha wafugaji wanajengewa mabirika na mabwawa ya kunyweshea mifugo kwani maji katika kipindi cha kiangazi yanakuwa machache ili wasiingie katika mito kunywesha mifugo yao. Pia kuanzisha sheria ndogondogo za vijiji zitakazosaidia kusimamia rasilimalia maji katika vijiji husika.

Ili kuhakikisha ulinzi madhubuti wa vyanzo vya maji, kamati za ulinzi na usalama katika mikoa na wilaya zishiriki kikamilifu kwa kushirikiana na ofisi za mabonde ya maji katika kulinda vyanzo vya maji. Hii itahusisha vyombo vya dola kufanya operesheni za kushtukiza mara kwa mara kwani hii itasaidia kupunguza ama kuondokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na watu kwenye nyanzo vya maji.

Baraza kama chombo cha kusimamia uhifadhi wa mazingira, limeshuhudia na kuona uharibifu na uchafuzi wa mazingira ukiendelea sehemu mbalimbali nchini na kusababisha athari mbalimbali kutokea. Vilevile Baraza limeendelea kujionea mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali yakifanyika, ukuaji wa miji na uanzishwaji wa miradi ukifanyika pasipo kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment). Vilevile, mipango mingi inaanzishwa pasipo kupitia mchakato muhimu wa tathimini za kimkakati ya mazingira (Strategic Environmental Assessment) kwenye mipango hiyo kama ilivyoainishwa kwenye Kifungu Na. 104 cha Sheria ya Mazingira.

Kwa kuzingatia umuhimu wa vyanzo vya maji na faida zake, Baraza linasisitiza kuhakikisha shughuli zote zinazoanzishwa kwenye maeneo hayo ziwe zimezingatia matakwa ya Sheria ya Mazingira ikiwa ni pamoja na kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa miradi inayoanzishwa, na vilevile kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo katika halmashauri iwe imefanyiwa Tathmini ya Kimkakati ya Mazingira na pia kuona jinsi gani sheria ya Mita 60 inazingatiwa kwenye vyanzo vya maji kama ilivyoainishwa kwenye Kifungu Na. 57 cha Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.