​TAREHE 15 JUNI MWISHO WA USAJILI KWA WAWEKEZAJI WA UCHENJUAJI MADINI


Kufuatia kubainika kwa athari mbalimbali za kimazingira zinazosababishwa na uchenjuaji wa madini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wawekezaji wote wanaojihusisha na shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu kuwa miradi yao inapaswa kuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) au Cheti cha Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit).

Akizungumza na waandishi wa habari leo hii Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka, amesema kuwa uwekezaji wowote unatakiwa kukidhi matakwa ya kisheria hususani katika suala zima la Tathmini ya Athari za Mazingira.

“Ifikapo tarehe 15 mwezi wa 6 wawekezaji wote wanatakiwa kuwa wameshakamilisha kusajili miradi yao kwenye ofisi za Baraza Makao Makuu, Mtaa wa Migombani Mikocheni Dar es Salaam. Au, katika Ofisi za Kanda zilizopo Mikoa ya Arusha, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Mtwara na Mwanza ili kupata cheti hicho.” Amesema Dkt.Gwamaka

Dkt. Gwamaka amesema kuwa wawekezaji wanapaswa kuwatumia wataalamu elekezi waliosajiliwa na Baraza walio zaidi ya mia nne (400) nchini watakaowasaidia katika ustawi wa miradi yao bila kuleta athari za kimazingira.

Kuhusu upatikanaji wa wataalamu elekezi Dkt. Gwamaka amebainisha kuwa orodha ya Wataalamu inapatikana katika Tovuti ya Baraza (www.nemc.or.tz) na orodha hiyo itatolewa kwa mara nyingine kwenye magazeti yatolewayo kila siku.

“Mtaalamu elekezi kazi yake ni kukuelekeza wewe mchimbaji ili uweze kujua kama ni vyanzo vya maji uvitunze vipi, kama ni maeneo ambayo unaharibu hadhi basi uweze kujua ni vipi utatunza mazingira”. Amesema Dkt. Gwamaka

Dkt. Gwamaka ameeleza kuwa kwa wale watakaoendelea kuendesha mitambo yao huku wakijua hawajakidhi taratibu watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani kwa kutaka kuharibu vyanzo vya maji pamoja na uchafuzi wa hewa.

“Sheria sisi kama baraza inatupa mamlaka ya kupiga faini, faini zipo kati ya milioni 5 hadi Bilioni 10, sio nia ya baraza kuweza kumpiga mtu faini kubwa ili afunge mradi wake. Baraza linawataka wote mzingatie sheria, wote mtunze mazingira kwa ustawi wa mwanadamu pamoja na watu wanaotumia rasilimali hizo waweze kupata haki zao.” Amesema Dkt. Gwamaka

Hatahivyo Dkt. Gwamaka amewataka wataalamu elekezi wanaofanya shughuli za athari kwa mazingira kutoza gharama zinazowiana na uhalisia wa shughuli husika pamoja na kuwa na mchanganuo wa gharama halisi ya kazi kwa maana ya gharama ya mahitaji kwa ajili ya tathmini na kaguzi na gharama itakayotakiwa ya utaalamu kwenye kazi hiyo.