NEMC YAIPONGEZA MAMLAKA YA BANDARI YA TANGA KWA KUZINGATIA TARATIBU ZA UTUNZAJI WA MAZINGIRA


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira amefanya ziara katika Mamlaka ya Bandari ya Tanga. Lengo kuu lilikuwa ni kukagua utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika utekelezaji wa ujenzi wa Mradi mpya wa kuongeza kina na kupanua Bandari ili kuruhusu Meli kubwa za mizigo kuweza kuingia na kutoka Tanzania.

Hata hivyo baada ya ukaguzi, Mkurugenzi ameonyesha kuridhishwa na mikakati mahsusi iliyowekwa kwa ajili ya kudhibiti uharibifu wa mazingira wakati wa ujenzi na wakati wa kuutumia mradi .

“Sisi kama NEMC tumejiridhisha na ujenzi unaoendelea kwa kuwa ujenzi huu unazingatia taratibu za kutunza mazingira, unatumia miundo mbinu ya kisasa ambayo ndio inayotakiwa na kujali afya za wafanyakazi. Hivyo, wamekidhi vigezo vya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004. Naomba niwapongeze Meneja pamoja na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya”

Aidha Mkurugenzi amewasisitiza watanzania wote kutumia bandari kwa ufasaha ili iweze kuleta tija Kitaifa kama vile kutoa fursa kwa wawekezaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza. Pia amesema kupitia mradi huu watu wengi wa karibu wamenufaika kwa kuuza vifaa vya ujenzi na kupata ajira hususani vijana.

“Lakini kubwa ambalo niendelee kulisisitiza ya kwamba fursa hii imekwisha kupatikana mahali hapa kama mnavyoona Bandari hii itakuwa na kina kirefu sana ina maana Meli nyingi kubwa zitaweza kufika mahali hapa, kwa hiyo tunaomba nchi za jirani pamoja na watanzania waitumie hii Bandari kwa ufanisi mkubwa ili iweze kuleta tija Kitaifa. Lakini kupitia mradi huu watu wa karibu wamenufaika kwa mfano kuleta madini ya ujenzi na vifaa vya ujenzi”

Pia Dkt. Gwamaka amewaondoa hofu wawekezaji wote, kutokuiogopa NEMC kwa kuwa haina nia mbaya na wawekezaji bali wana lengo la kuwajengea uelewa na kutoa ushauri wa Kitaalamu ili waweze kwenda sambamba na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kwa ustawi wa mazingira.

“NEMC hatupo kwa ajili ya kuadhibu bali tupo kwa ajili kufundisha na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu utunzaji wa mazingira ili mazingira yetu yaweze kuwa salama kwa kizazi cha sasa na cha baadae”

Naye Kaimu Meneja wa Bandari Bwana Donald Ngaile amedhihirisha kwamba katika hatua za utekelezaji wa miradi ya Bandari suala la utunzaji wa mazingira wanalipa kipaumbele na ndiyo maana wanafanikiwa kutekeleza Sheria ya mazingira.

“Siri kubwa ya mafanikio katika utunzaji wa mazingira wakati wa utekelezaji wa miradi ya Mamlaka ya Bandari ni kutii Sheria bila shuruti”.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji Sheria na utekeleaji wa Sheria ndugu Thobias Mwesiga amemaliza kwa kuishukuru Mamalaka ya Bandari kwa kuendesha shughuli zake sambamba na kuzingatia viwango vya utunzaji wa mazingira kama kuweka mikakati madhubuti ya kuthibiti uchafuzi wa mazingira wakati wa kupokea kemikali mbalimbali na mafuta.