KATAZO LA MIFUKO YA PLASTIKI NA HALI YA MATUMIZI YA MIFUKO MBADALA


KATAZO LA MIFUKO YA PLASTIKI NA HALI YA MATUMIZI YA MIFUKO MBADALA
Mifuko ya plastiki ni aina ya mifuko yenye mchanganyiko wa kemikali zisizooza hivyo kuleta athari kwenye mazingira pamoja na afya kwa binadamu na Wanyama.
Inakadiriwa kuwa, matumizi ya mifuko ya plastiki duniani ni bilioni 500 mpaka trilioni moja na nchini Tanzania, tani 350,000 ya mifuko ya plastiki huzalishwa kila mwaka ambapo hii ni chini ya asilimia kumi (10%) ya mifuko iliyotumika hurejereshwa. Kutokana na tafiti mbalimbali mifuko ya plastiki huchukua miaka 400 mpaka 1000 kuoza ardhini.
Athari mbalimbali zitokanazo na mifuko ya plastiki zimeweza kushuhudiwa kama;
 Kuathiri mifumo ikolojia ya bahari ambapo Inakadiriwa 100,000 viumbe bahari na ndege bahari millioni moja kila mwaka wanakufa kwa kula mifuko ya plastiki).
 Kuchafua miji kutokana na kushindwa kuoza
 Kuathiri mifugo ambapo ranchi ya Kongwa mkoa wa Dodoma Ng’ombe 57 walikufa mwaka 2017 kutokana na kula mifuko ya plastiki.
 Kuharibu miundombinu kwa kuziba kwenye mifereji na baadhi ya njia za maji.
 Kubeba na kusambaza viumbe vamizi na bacteria
 Inapochomwa moshi wake unamadhara (casinogenic compounds) na unaweza kusababisha maradhi ya kansa



Kutokana na madhara ya mifuko ya plastiki, Serikali ilitoa tamko la kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki mnamo tarehe 1 Juni, 2019 na kuandaa Kanuni ya Usimamizi wa katazo la Matumizi ya Mifuko ya Plastiki iliyotoka kwenye Gazeti la Serikali Na. 394 ( The Environmental Management (Prohibition of Plastic Carrier Bags) Regulation, 2019, which made under section 230 (2) (f) of the Environmental Management Act, Cap 191))
Kwa mujibu wa Kanuni, ni marufuku kutengeneza, kuuza, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.
Lengo la Serikali kutengeza kanuni hiyo ni kutokana na athari mbalimbali zitokanazo na mifuko hiyo kama: kuziba mitaro ya maji, kuwa kero kwenye madampo na kusambaa kwenye mazingira nchini kote, kuharibu ubora wa ardhi ya kilimo, kuwa na athari kwa viumbe wa baharini na nchi kavu na baadaye kwa binadamu.
Muitikio wa utekelezaji wa sheria hii ni pamoja na matumizi ya mifuko mbadala kwa ajili ya kubebea bidhaa. Aidha, pamoja na matumizi ya mifuko mbadala kumekuwa na changamoto za ubora wa mifuko hiyo mbadala. Hali hiyo imepelekea mahitaji ya utafiti wa kujua sifa za mifuko hiyo na uwezo wake wa kuoza inapokuwa kwenye mazingira. Hii ni kuisaidia serikali kuwa na maamuzi sahihi juu ya mifuko mbadala inayotakiwa kutumika pasipo kuathiri mazingira. Ili kufanikisha azma hiyo ilioonekana kuna umuhimu wa kushirikisha wadau kwenye tafiti zenye kuainisha sifa za mifuko mbadala, viasilia vinavyotumika kutengenezea na uwezo wa mifuko hiyo kuoza inapokuwa kwenye mazingira.
Hivyo, kwa ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), NEMC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inafanya tafiti ya ‘Study of Non-Woven Carrier Bags Manufactured and/or marketed in Tanzania to Determine the Physical and Chemical Characteristics.’ Wadau wengine katika utafiti huu ni pamoja na Kitivo cha Kemia na Kitivo Cha Uhandisi wa Madawa na Usindikaji, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Taasisi ya Tafiti na Maendeleo kwa Viwanda (TIRDO); na Shirika la Viwango la Taifa (TBS). Aidha, wataalam kadhaa kutoka taasisi hizo wameainishwa kwa ajili ya zoezi zima la utafiti wa sifa za mifuko mbadala (non-woven) inayotumika kwa sasa.