Waziri Zungu atoa siku 10 kupata ripoti ya athari katika bwawa la kidatu


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azzan Zungu amewapa siku kumi wataalum wa Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa mazingira(NEMC), TANESCO na wadau wengine kufanya tafiti na kutoa ripoti ya tathmini ya athari kwa mazingira kufuatia kuongezeka kwa maji kupita kiasi katika mabwawa ya kufua umeme.

Waziri Zungu ameyasema hayo alipofanya ziara ya pamoja na Waziri wa Nishati,Dkt. Medard Kalemani iliyolenga kujionea hali ya bwawa la kidatu ilivyo kufuatia kujaa maji kupita kiasi jambo lilosababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo baada ya kurudi maji hayo kupita.

“Muhimu kufanya tafiti juu ya athari zilizojitokeza kutokana na kuongezeka kwa maji kwenye mabwawa ikiwa ni pamoja na kupima kiwango cha mapote,” alisema Waziri Zungu

Akifafanua zaidi, waziri Zungu alisema inawexekana mabwawa yakawa yamejaa matope kwa chini hivyo swala la kuyafungulia maji isije leta tatizo la kushindwa kuzalisha umeme kwa kiwango kinachotakiwa.

“Mradi wa umeme mto Rufiji unategemea uwepo wa maji ya kutosha kutoka katika vyanzo hivyo vya maji na kuna kila sababu ya kufanya tafiti ili kivilinda vyanzo hivyo ili maji yakalijaze bwawa hilo,” alisema Waziri Zungu.

Alisema Wizara yake ndiyo yenye thamana na mazingira hivyo itahakikisha mazingira katika vyanzo vyote vya maji vinalindwa na kuhifadhiwa ili kuwa na uhakika wa maji ya kuendesha uzalishaji wa umeme katika Bwawa la mto Rufiji.

“Serikali imewekezeka fedha nyingi kuhakikisha ujenzi wa mradi wa umeme mto Rufiji unakamilika hivyo ni jukumu letu sasa kufanya mradi huu unakuwa endelevu kwa kutunza vyanzo vya maji,” alisema Waziri Zungu.

Alisema elimu kwa wananchi iendelee kutolewa hususani ya kufanya shughuli za kiuchumi kando au pembezoni mwa mwa mito na vyanzo vya maji ili kutoathiri upatikanaji wa maji kwenye mabwawa ya yanayozalishaji wa umeme.

“Rai yangu kwa wananchi ni kuendelea kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji jambo litakalosaidia uzalishaji wa umeme kuongezeka na kuifanya nchi kupiga hatua zaidi ya maendeleo ya kiuchumi,” alisema.

Kwa upande, Waziri wa Nishati,Dkt.Medard Kalemani amesema tayari Wizara yake ilishaunda kamati ya kufanya tathmini hiyo ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na maji yanayopatikana yakawezeshe bwawa kubwa la mto Rufiji linapata maji kwa ajili ya kuzalisha umeme megawatt 2,115.

“Maji yanayohitajika katika bwawa la Rufiji ni zaidi ya mita za ujazo bilioni 32 hivyo ni muhimu vyanzo vya maji vilindwe kikamilifu,” alisema Waziri Kalemani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw.Loata Sanare alisema serikali ya mkoa imeshaanza kutoa elimu kwa wananchi na kuwataka wote waliojenga kando ya mto kuhama ili kuepukana na majanga ya mafuriko.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC,Dkt.Samuel Gwamaka alisema Baraza limepokea maelekezo ya Waziri na tayari timu ya wataalum ipo kazini kuhakikisha ripoti ya tathmini ya mazingira inakamilika katika muda uliopangwa.

Kamati iliyoundwa itaongozwa na Karibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na kuunganisha Wizara ya Ardhi,NEMC,TANESCO, Wasimamizi wa Bonde la Mto Rufiji pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo ili kutoa tathmini ya hali ya mabwawa ilivyo na namna ya kutunza mazingira kwa ujumla.