WAZIRI JAFO AZIAGIZA MAMLAKA HUSIKA KUFANYA TATHIMINI YA MILIMA ILIYOPO KATIKA JIJI LA DODOMA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Tume ya Madini pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya tathimini yah ali ya kimazingira iliyopo katika milima yote ndani ya Jiji la Dodoma kwa kipindi cha wiki mbili kuanziaMachi 14,2024.

Agizo hilo limekuja mara baada ya kutembelea eneo la Iyumbu Kata ya Iyumbu Jijini Dodoma na kutoridhishwana hali ya uharibifu wa mazingira unaosababishwa nauchimbaji wa madini ujenzi katika eneo hilo.

"Kwanza kabisa sijaridhishwa na hii hali hapa, nawaagiza NEMC, Tume ya Madini na Jiji fanyeni tathimini ya milima yote ya Jiji la Dodoma lakini pia fuatilieni Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 inayozungumzia kati ya NEMC, Jiji na Tume ya Madini ambao ndio wanaotoa vibali, ili tuone maeneo haya yote ili tuyatangaze kuwa maeneo ya kuyahifadhi na tusipofanya hivi baadae haitaonekana Dodoma ile tunayoijua." Amesema Waziri Jafo.

"Inawezekana hivi vichuguu vyote kila mtu ana kichuguu chake anachimba, Sheria inakataza na nawapa wiki mbili nataka taarifa ya tathimini na ushauri nini kifanyike." Ameongezea Waziri Jafo.

Akihitimisha Ziara yake hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo amewataka wataalamu hao wa NEMC, Tume ya Madini na Jiji la Dodoma kuhakikisha taarifa yao inajikita katika tathimini, idadi ya milima iliyopo jijini Dodoma, hali ilivyo pamoja na ushauri wa nini kifanyike