​TANI 2 ZA TAKA ZA MAJUMBANI ZAKUSANYWA NA WANAWAKE WA NEMC ENEO LA MIKOKO KIGAMBONI.


Tani mbili (2) za taka za majumbani zilizohusisha pampas, chupa za plastiki, mabati, mabox na mifuko ya plastiki zimekusanywa na wanawake watumishi wa NEMC eneo la mikoko lililopo Mtaa wa Kibugumo, Kata ya Mji Mwema Wilaya ya Kigamboni katika zoezi la usafi lililofanywa na wanawake hao ili kuenzi kaulimbiu ya mwaka 2024 isemayo " Wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya Taifa".

Akizungumza katika zoezi hilo lililohusisha wadau wa mazingira kutoka Hudefo, Teemo, Manispaa ya Kigamboni, BMU na Silk Kot Meneja wa Tafiti za Mazingira kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Bi. Rose Salema amesema uchafuzi wa fukwe na uharibifu wa mikoko huathiri mazalia ya viumbe hai na kusababisha mikoko kupoteza uwezo wa kuchuja taka zisifike baharini na kuathiri ustawi viumbe hai, uchafuzi wa hali ya hewa na mandhari ya eneo husika.

Amewataka wananchi kutambua fursa iliyopo katika kuzitenga taka kuanzia majumbani ili kuepuka utupaji holela katika maeneo yasiyo rasmi pamoja na fukwe hali inayopelekea uharibifu wa Mazingira na viumbe wa majini.

Naye Kaimu Meneja Kanda ya Mashariki Kusini Bi. Lilian Kapakala alipozungumza amekemea vikali wakandarasi bubu wanaochafua fukwe kwa kutupa taka za majumbani hali inayopelekea uharibifu wa mazingira.

Katika hatua nyingine wanawake hao wa NEMC wamepanda Miche 100 ya mikoko ili kulinda kingo za bahari na kutunza mazingira