NEMC YAELIMISHA UMMA UDHIBITI WA KELELE CHAFUZI NA MITETEMO
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuimarisha juhudi za kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo kufuatia ongezeko la malalamiko katika maeneo ya mijini na vijijini.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Bw. Hamadi Taimuru, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC), amesema kelele zimeendelea kuwa changamoto kubwa kwa afya na ustawi wa wananchi kutokana na shughuli za burudani, ujenzi, biashara na matumizi ya vifaa vya sauti vinavyokiuka viwango vya kisheria.
Bw. Taimuru amefafanua kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Sura 191) na Kanuni za Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za mwaka 2015 zimeweka viwango maalumu vya kelele kwa maeneo ya makazi, biashara, viwanda na Taasisi muhimu kama Hospitali na shule, sambamba na kuainisha utaratibu wa utoaji vibali kwa shughuli zinazoweza kusababisha kelele kubwa.
Amesema athari za kelele za muda mrefu ni pamoja na kupoteza usikivu, msongo wa mawazo, shinikizo la damu na kuathiri umakini wa watoto shuleni, hivyo kulifanya suala la udhibiti kuwa muhimu kwa kulinda afya ya umma".
Aidha, amebainisha uwepo wa changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Kanuni za udhibiti, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kupimia kelele kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, uelewa mdogo wa wananchi kuhusu athari za kelele, pamoja na baadhi ya biashara na maeneo ya burudani kutokufuata sheria na muda wa utulivu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viwango vinavyoruhusiwa ni 70dBA mchana na 60dBA usiku kwa maeneo ya viwandani; 50dBA mchana na 35dBA usiku kwa makazi, 60dBA mchana na 50dBA usiku kwa makazi yenye viwanda vidogo, 55dBA mchana na 45dBA usiku kwa maeneo ya makazi, biashara na burudani; na 45dBA mchana na 35dBA usiku kwa Hospitali, Shule, Kumbi za mikutano na maeneo ya mapumziko.
Katika kuimarisha usimamizi, Bw. Taimuru alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya OSHA, Polisi, BASATA, Serikali za Mitaa, nyumba za ibada na wamiliki wa kumbi za burudani katika kutekeleza majukumu yao, ikiwemo kusimamia vibali, kutoa elimu, kuhakikisha matumizi sahihi ya vifaa vya sauti na kufanya kaguzi za mara kwa mara.
Aliongeza kuwa ramani za viwango vya kelele, kampeni za uelimishaji na mifumo rahisi ya utoaji taarifa za malalamiko ni hatua muhimu zinazohitajika kuimarishwa.
Akihitimisha, Bw. Hamadi Taimuru amesema Tanzania ina mfumo madhubuti wa kisheria wa kudhibiti kelele na mitetemo, na kwamba ushirikiano wa wadau wote, sekta binafsi, Taasisi za umma na wananchi ni msingi muhimu wa kulinda afya, utulivu na ustawi wa jamii.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15

