​NEMC YATOA WITO KWA WANANCHI KUTENGANISHA TAKA KUTOKA KWENYE CHANZO ILI KULINDA MAZINGIRA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kutenga taka kutoka kwenye chanzo hasa hatarishi na taka ngumu ili kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.

Wito huo kwa wananchi, umetolewa na Mhandisi wa Taasisi hiyo Bi.Beatitude Sizya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la NEMC la maonesho lililopo viwanja vya sabasaba kwenye Maonyesho ya 48 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea jijini hapo.

Bi.Beatitude amesema kuzichanganya taka pamoja kunaweza kuathiri afya na uchafuzi wa mazingira kwani kila taka inao utaratibu wake wa kuteketezwa ili kulinda mazingira.

"Tunatoa elimu kwa wananchi kujenga utaratibu wa kuzitenga taka hatarishi na ngumu kwa usalama wa kulinda afya zao.Lakini kama kuna taka ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu tunawakaribisha ofisi watuelezee kisha tuwashauri na kuwapa mbinu jinsi ya kuteketeza.," amesema.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi, Sosholojia kutoka NEMC, Bi.Suzan Chawe amesema mchakato wa kupata cheti cha tathimini ya mazingira kwa sasa hufanyika kwa haraka na wazi kwakuwa shughuli zote zinafanyika kupitia mtandao.

"Shughuli zote zinafanyika kwa mfumo mtandao na inakuwa rahisi kwa mwananchi kufutilia hatua kwa hatua na vilevile ni rahisi kupata mrejesho au majibu kama kuna shida katika maombi yako au baraza bado linahitaji nyaraka kutoka kwa muombaji," amesema

Katika hatua nyingine wawekezaji na wamiliki wa miradi ya uendelezaji wametakiwa kulipa ada ya uhifadhi wa mazingira ili kuiwezesha Taasisi hiyo kufanya shughuli zake za Tathimini ya Athari kwa Mazingira kwa wakati na weledi.

Akikazia suala la ada hiyo, Afisa mtendaji Mkuu NEMC, Bi Marlene Moshi amesema kulipwa ada hiyo kwa wakati inawawezesha watendaji wa Taasisi hiyo kuwatembelea na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira.

Akitangaza muda wa kuanza kulipa ada hiyo, Juni25,2024,Msimamizi wa ada na tozo kutoka NEMC, Bw. Canisius Karamaga alisema utaratibu wa ada hiyo hulipwa mara moja kwa mwaka kuanzia Julai mosi hadi Desemba 31 kila mwaka.

“Unaweza kulipa hapa katikati Agosti,Oktoba lakini mwisho lazima iwe Desemba 31 na baada ya hapo ikitokea mtu hajalipa baada ya muda huo kuanzia Januari hadi Juni ya mwaka wa fedha itaambatana na adhabu ya asilimia tano ya fedha,” alisema

Awali, katika mkutano huo, Meneja Mawasiliano kwa Umma kutoka NEMC, Bi.Irene John amesema Taasisi hiyo kwakuwa imepewa jukumu hilo la usimamizi na Uhifadhi wa mazingira shabaha yake ni kuona mazingira yanaendelea kuwa rafiki.