NEMC YAKABIDHI MAJIKO YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA SHULE YA MSINGI ARUSHA


Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo tarehe 7 Machi, 2025 limekabidhi majiko manne ya Nishati Safi ya kupikia (Gas stoves) kwa Shule ya Msingi Arusha inayotoa huduma ya chakula kwa wanafunzi takribani 1,600 ambapo majiko hayo yana uwezo wa kupika chakula chenye ujazo wa Lita 700 ambapo majiko matatu kati ya hayo yana uwezo wa kupika chakula cha ujazo wa Lita 200.

Akizungumza katika hotuba yake Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (NEMC) Bi. Liliana Lukambuzi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu NEMC amesema, "Matumizi ya mkaa na kuni (nishati chafu) yanayochangia uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti, kuathiri afya ya jamii kutokana na moshi (hasahasa wanawake na watoto ambao hutumia muda mwingi jikoni) na pia kupelekea kuongezeka athari za mabadiliko ya tabianchi".

Ameongeza kuwa majiko hayo yaliyokabidhiwa katika shule hiyo yatasaidia wapishi kukamilisha majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kwa wakati na pia yatasaidia kuboresha afya na ustawi wa wanafunzi na taifa kwa ujumla.

Zoezi hili linaunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika. vilevile ni katika kutekeleza mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa mwaka jana 2024 unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya kupikia.