​NEMC KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KUJIRIDHISHA UHIFADHI WA MAZINGIRA KWA MUJIBU WA SHERIA YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeanza utaratibu wa kupitia miradi yote iliyopatiwa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) ili kujiridhisha kama wamiliki wa miradi hiyo wanatekeleza matakwa ya kisheria yaliyoainishwa kwenye vyeti hivyo wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa Sheria NEMC Bw. Hamadi Taimuru alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mwenendo wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa Sheria katika eneo la Tathmini ya Athari kwa Mazingira.

Bw. Taimuru amesema Baraza limefikia uamuzi huo baada ya kuona miradi mingi haifuati masharti yaliyoainishwa kwenye vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kuhakikisha kwamba Mazingira yanaendelea kutunzwa wakati wa utekelezaji wa mradi na baada ya kukamilika kwa mradi.

“Tumeandaa mkakati wa kuwafuata mmoja mmoja kukagua na kujiridhisha matakwa ya cheti na wao wanafanya nini kwa lengo la kuhakikisha mazingira yetu yanaendelea kuwa safi na salama na wananchi wakae katika mazingira yenye afya na hata kazi zao ziweze kwenda vizuri” Amesema Bw. Taimuru.

Akizungumzia kuhusu kaguzi za kila mwaka za mazingira Bw. Taimuru amesisitiza wawekezaji kujikagua na kuwasilisha taarifa zao Baraza ili zipitiwe na kujiridhisha huku akiwashukuru wawekezaji waliokwisha kufanya hivyo na tayari taarifa zao zimeshapitiwa na Baraza na kujibiwa kwa mujibu wa Sheria.

Naye Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Bi. Irene John amesisitiza kuwa Baraza litaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kufanya Tathimini ya Athari kwa Mazingira kabla ya kuanza miradi ili Tanzania iendelee kuwa salama kwa wageni, wenyeji , wanyama na hata vizazi vijavyo kwamaendeleo endelevu ya Taifa letu