NEMC KANDA YA KASKAZINI YABAINISHA NAMNA ILIVYOSIMAMIA MIRADI

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kanda ya Kaskazini limetaja mafanikio kadhaa yaliyopatikana ndani ya miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2024 kuwa ni pamoja na kusimamia na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya afya 1286.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Meneja wa Kanda ya Kaskazini inayohudumia Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Benjamini Dotto, alisema ndani ya kipindi hicho Baraza limetekeleza majukumu ya kusimamia uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Alitaja moja ya shughuli zilizofanyika kwa sekta ya afya ni kushirikiana na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) na jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kusimamia uteketezaji wa dawa za binadamu zilizokwisha muda kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini-Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC).
Aidha, alisema NEMC Kanda ya Kaskazini inasimamia Sera na Sheria za Mazingira na inahakikisha kuwa uchumi wa nchi unakua sambamba na uhifadhi wa mazingira.
Hivyo, kusimamia utunzaji wa mazingira katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo; Miradi ya huduma za afya. Kanda ya kaskazini inasimamia jumla ya miradi ya afya 1286, kiutalii ni 317, nishati ni 247, viwanda vya mbao ni 201, uwekezaji katika viwanda 176, kilimo ni 118, ghala za kuhifadhia bidhaa, vifaa au mali nyingine ni 74. "Miradi ya ujenzi ni 27, uchimbaji wa madini ni 26, wakulima wa mifugo ni 12, ujenzi wa majengo ni 11, mawasiliano ni 5, miundombinu ni 3,"alisema.
Aidha alieleza kuwa NEMC Kanda ya Kaskazini imefanikiwa kusimamia Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa miradi mikubwa kama barabara, viwanda na migodi.
Awali, alibainisha kuwa Baraza hilo limekuwa likiratibu na kuunganisha vyombo mbalimbali vya Serikali katika masuala yanayohusiana na Usimamizi na Uhifadhi wa mazingira kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 na Kanuni zake. "Kuhakikisha miradi ya maendeleo kabla ya kutekelezwa inafanyika Tathmini ya Athari kwa Mazingira au kwa iliyopo inafanyiwa Ukaguzi wa Awali wa Mazingira, ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya miradi hiyo ili kupata Cheti cha Mazingira "alisema.
Alisema Kanda ya Kaskazini imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii na Mifumi Ikolojia nyeti yenye umuhimu Kitaifa na Kimataifa. "Maeneo haya ni pamoja na Maeneo yaliyohifadhiwa kama vile Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Hifadhi za Taifa za Tarangire, Mkomazi, Kilimanjaro, Ziwa Manyara na Arusha. Hii pia inahusisha maeneo kadhaa yanayohifadhiwa kama vile Mapori Tengefu, Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii na Misitu ya Hifadhi,"alisema.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15