‚ÄčMIZAMBARAU 3000 YAPANDWA MTO TEGETA


Miti 3000 aina ya mizambarau imepandwa katika mtoTegeta uliopo Kata ya Goba Wilaya ya Ubungo Mkoa wa Dar es salaam.

Miti hiyo imepandwa Aprili 17,2024 na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Jumuia ya Maridhiano (JMAT) kwa lengo la kuimarisha mazingira ya vyanzo vya maji ili kudhibiti mafuriko yanayotokea na kusababisha maafa katika jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo Bi. Beatrice Mbawala amesema miti hiyo itasaidia kudhibiti janga la mafuriko linaloweza kutokea kwa sababu ya kutanuka kwa mto Tegeta.

Naye Kaimu Meneja (NEMC) Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bw. Andrew Ugolole alipozungumza amewasisitiza wananchi wote kuiga mfano wa JMAT kwa kupanda miti kwa wingi hasa msimu huu wa mvua ili kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.