MIAKA MINNE YA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, NEMC YABAINISHA MAKUBWA YALIYOFANYIKA


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita Baraza limesajili jumla ya miradi 8,058, ambapo kati ya hiyo, 5,784 ni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na 2,274 ni ya Ukaguzi wa Mazingira. Vikao 3,836 vya wataalam vilifanyika kwa ajili ya kufanya mapitio ya taarifa za TAM na Ukaguzi wa Miradi na kutoa mapendekezo ya maboresho ya masuala ya msingi ya kuzingatiwa katika taarifa hizo.

Aidha Miradi 4,570 iliidhinishwa na kupewa vyeti vya mazingira. Kati ya hivyo, 3,058 ni vya TAM, 765 ni vya Ukaguzi, huku vyeti vingine vikiwemo vya kubadili masharti 169, vyeti vilivyohamishwa umiliki 552, vyeti vya muda (PEC) 53 na cheti kilichorudishwa (certificate of surrender) 1.

Ameongeza Kwa kusema "Katika kipindi cha mwaka 2020/21- 2024/25, Baraza limefanikiwa kusajili wataalam elekezi wa Mazingira 1,023 na kutoa vyeti vya utendaji kwa Wataalam Elekezi 503 baada ya kukidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili na utendaji wa Wataalam Elekezi wa Mazingira za mwaka 2021. Kanuni hizi mpya zimeongeza ufanisi kwa kuruhusu usajili kufanyika wakati wowote. Usajili wa Wataalam Elekezi wa Mazingira unafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki ambao umeongeza ufanisi wa kushughulikia maombi."

Akizungumza kuhusu Uhamasishaji na utoaji wa elimu Dkt. Semesi ameeleza "Baraza limefanikiwa kuandaa vipindi 88 vya uhamasishaji kupitia vyombo vya habari na mikutano 20 ya wadau kuhusu madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki. Vilevile, kaguzi zilifanyika katika maeneo 178 ya uzalishaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki, ambapo maeneo 57 yalikutwa na makosa na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria. Zaidi ya Tani 150 za vifungashio visivyokidhi viwango vilikamatwa, vikataifishwa na kuteketezwa kwa mujibu wa Sheria."

Dkt. Immaculate Sware Semesi leo Machi 24,2025 amezungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dodoma kueleza Utekelezaji wa Majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kwa kipindi Cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita.