MHE.WAZIRI ZUNGU AZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI YAPENDEZESHA TANZANIA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe.Mussa Azzan Zungu amezindua rasmi kampeni ya upandaji miti Nchi nzima inayoitwa pendezesha Tanzania, itakayoendeshwa na Benki ya CRDB ikishirikiana na ofisi ya Makamu wa Rais na TAMISEMI. Kampeni hiyo ilizinduliwa kwa kupanda miti katika viwanja vya shule ya Msingi Goba iliyoko Jijini Dar es Salaam leo hii.

Katika zoezi hilo lilojumuisha wadau mbalimbali wa Mazingira, Mhe.Zungu aliambatana na wawakilishi kutoka ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC. Mhe. Zungu ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha Kampeni hii na aliongeza kusema kuwa CRDB kufanya zoezi la upandaji miti kwa kushirikiana na wanafunzi wamefanya jambo la msingi kwani hivi ndio vizazi vijavyo na vinahitaji mazingira safi na salama.

Zoezi la upandaji miti shuleni hapo lilishirikisha wanafunzi wa shule mbalimbali na wadau wa mazingira wakiwakilisha wananchi wa eneo la Goba na Taasisi mbalimbali. Akiwa katika zoezi hilo Mhe. Zungu amesisitiza juu ya upandaji na utunzaji wa miti kwani tunapokata miti tunaharibu mazingira yetu, ameeleza kuwa takribani asilimia 76 ya wananchi vijijini wanatumia maliasili kwa maisha yao na asilimia 95 ya nishati wanayotumia imetokana na miti, hivyo ukataji miti ni sehemu kubwa sana ya kuharibu mazingira katika Taifa letu.

“Watu wengi hawaelewi wanafikiri mazingira ni taka ngumu, maji taka au chupa za plastiki tu, mazingira ni kila kitu kinacho tuzunguka,hivyo tujitahidi kupanda miti ili kuiweka nchi yetu katika usalama. Wanafunzi na watu wengi hawaelewi kuwa juhudi kubwa zinazofanywa na serikali za kulinda mazingira imesaidia barafu katika mlima Kilimanjaro sasa hivi kuongezeka lakini barafu hiyo inaweza kupotea kutokana na kukata miti hovyo”

Ameendelea kusisitiza kuwa jitihada kubwa za Serikali ambazo zinafanywa kulinda mazingira ziungwe mkono na wananchi kwa ni jukumu la kila mmoja na sio kuitegemea NEMC peke yake. Hata hivyo Mhe. Zungu ameipongeza CRDB kwa namna wanavyoiangaikia jamii na kutoa ushirikiano kwenye afya, mazingira, elimu na michezo.

“Kutokana na juhudi zinazofanywa na Benki hii nawateua CRDB kuwa mabarozi wa mazingira na watakabidhiwa rasmi cheti chao, ili nawao waonemchango wao unavyogusa nyoyo za watanzania na wapenda mazingira” alisema Mhe. Zungu

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakari Kunenge, amesema kuwa kama mnavyofahamu katika jiji la Dar es Salaam hali ya Tabianchi inabadilika, hivyo wazo la upandaji miti katika jiji hili ni zuri sana kwani itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi. Ameendelea kusema kuwa biashara na mapato yanayopatikana CRDB yanatokana na jiji la Dar es Salaam hivyo juhudi zao za kupanda miti ni kufanya mji huu uwe safi na mazingira yanayovutia.

Naye Mkurugenzi Mtendaji CRDB Abdulmajid Nsekela ameeleza kuwa kampeni hii ya Pendezesha Tanzania inatokana na kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali yetu katika kuboresha ustawi wa Taifa letu. Uzinduzi wa kampeni hii ya Pendezesha Tanzania ni muendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya Benki ya CRDB Katika kutunza na kuboresha mazingira.

“ Tunafanya hivi tukiamini kuwa mazingira bora yanamchango mkubwa sana katika ustawi wa jamii yetu na maendeleo yetu kwa ujumla. Hii pia imetufanya kuboresha mfumo wetu wa biashara ambao unazingatia utunzaji wa mazingira kwa kupunguza huduma zinazohitaji makaratasi”

Hata hivyo akiwa katika harakati za kampeni za kimazingira Mhe. Zungu pia ameshirikiana na Manispaa ya Ilala, Taasisi isiyo ya kiserikali ya Nipe Fagio pamoja na kampuni ya Green Waste kusafisha pembezoni mwa Bahari katika daraja la Salenda Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya usafi Duniani. Ameeleza kuwa uchafu uliopo katika eneo hilo hauzalishwi hapo bali unatoka maeneo ya mto msimbazi na sehemu nyingine, hivyo kuna haja ya uchafu huo kutolewa kwani ukiachwa urudi Baharini utaendelea kusababisha madhara kwa viumbe vilivyomo majini.

Mhe. Zungu amewataka watanzania waache tabia ya kutupa taka hovyo wakiwa kwenye magari kwani kufanya hivyo ni makosa kisheria na inaharibu mazingira yetu kwa ujumla kwani mji unapokuwa msafi unafanya kuwa kivutio cha watalii na inaleta ustawina viumbe hai vyote.