JUKWAA LA USIMAMIZI WA BAHARI TANZANIA LAZINDULIWA RASMI


Jukwaa la Usimamizi wa Bahari Tanzania lenye lengo la kuleta wadau mbalimbali wa bahari pamoja ili kujadili na kuendeleza sera za usimamizi wa bahari nchini limezinduliwa leo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe. Zahor Kassim Mohamed katika hoteli ya Serena iliyopo Jijini Dar es salaam.

Akizindua jukwaa hilo lililohudhuriwa na wadau mbalimbali pamoja na viongozi wa Serikali amesema lengo mahususini kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari na kukuza uchumi wa buluu kwa njia endelevu ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto zinazokumba mifumo ya bahari, kama vile uvuvi haramu, uchafuzi wa mazingira, na mabadiliko ya tabianchi na kusisitiza haja ya kuunganisha Sera za kitaifa na mifumo ya utawala wa bahari ya kimataifa ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, hasa lengo la 14 la Umoja wa Mataifa kuhusu maisha chini ya maji.

Amesema “tumeanzishajukwaa hili ili kushirikisha wadau mbalimbali wanaoshughulika na masuala ya bahari, kama mnavyofahamu bahari ina matumizi mengiyakiwemo uvuvi, mafuta, gesi, masuala ya madini, usafiri wa baharini, kilimo na utalii. Katika nchi yetu, kila sekta inasimamia masuala yake binafsi bila kushirikisha wengine, kwahiyo tumewakutanisha wadau hawa ili tuweze kufanya kazi pamoja.”Mhe. Zahoro Kassim.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipozungumza amesema jukwaa hili litatoa fursa ya kujadili masuala muhimu yanayohusu utawala wa bahari, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, jamii za Pwani, na sekta binafsi katika usimamizi wa rasilimali za bahari.

“Tanzania tumebarikiwa kuwa na rasilimali muhimu sana ukanda wa pwani, bahari yetu ni kubwa na eneo la bahari tunalolimiliki ni takribani km 200,0000 na hata urefu wa ukanda wa pwani kuanzia Tanga hadi Mtwaraunazidi km 1000, sasa hatujaitumia inavyotakiwa.” Amesema Dkt. Immaculate Semesi.

Ameainisha changamoto za bahari kwa sasa kuwa ni uvuvi uliopita kiasi katika maeneo madogo, uharibifu wa mazingira maeneo ya pwani, watalii wanazidi maeneo ya pwani, kukata mikoko ambayo ni muhimu katika kuhakikisha bahari inaleta tija na kutoa wito kwa nchi zote duniani kufanya kazi kwa karibu ili kuboresha sheria na sera zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira ya bahari, kwa kutumia utafiti wa kisayansi na mbinu bora za usimamizi kwa maendeleo endelevu ya mazingira.

Mkutano huo, uliohusisha wataalamu na viongozi wa mazingira kutoka maeneo mbalimbali, umejikita katika kutafuta suluhu za kimataifa kuhusu changamoto za mazingira zinazokumba bahari na mikoa ya pwani lakini pia kulijadili masuala muhimu kama vile uchafuzi wa bahari, uvuvi haramu, na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mazingira ya bahari.

Washiriki waliojumuika kwa lengo la kuunda mikakati ya pamoja ya kulinda na kudumisha usawa wa mifumo ya bahari na majiji ya pwani ni pamoja na Wizara ya uchumi wa buluu Zanzibar, TAMISEMI, TFS, TAFICO, AZAM Marine, WWF, TASAC,TPDC, ZEMA, Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), wavuvi pamoja na wadau wengine wa Mazingira.