Zungu ataka ushauri wa kitaalamu kutatua mzozo hoteli za fukwe ya Dar


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuteua wataalam wa mazingira ili waeleze sababu halisi za uharibufu unaotokana na mawimbi makubwa na kuwa chanzo cha mzozo kati ya hoteli za Kunduchi na White Sand.

Waziri Zungu amewapa wataalamu hao siku nne kuanzania jana na kuwataka wawasilishe taarifa yao kwake ifikapo leo..

Akizungumza mara baada ya kutembelea fukwe ziliko hoteli hizo mbili mwishoni mwa wiki Waziri Zungu amesema anaamini mabadiliko ya tabia nchi ndiyo sababu ya msingi ya uharibufu wa fukwe na chanzo cha mzozo baina ya hoteli hizo.

“Mabadiliko ya tabia nchi yanapelekea kuibuka kwa athari tunazoziona katika fukwa zetu. Kukabiliana na hali hiyo tunahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali, Sekta Binafsi pamoja na wadau wa Mazingira kwa ujumla,’’ amesema Bw. Zungu

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ili kuvutia wawekezaji ikiwemo suala la amani na utulivu lakini akawataka wawekezaji kote nchini kuzingatia kanuni na sheria za mazingira.

“Tusingependa kuwa sehemu ya migogoro. Sisi kama serikali kazi yetu ni kuhakikisha amani na utulivu pamoja na kuleta suluhu za kudumu na kuchochea uwekezaji hapa nchini,’’ ameleza.

Waziri Zungu ametembelea eneo hilo kwa sababu Wellworth Hotels & Lodges Ltd, wanamiliki Hoteli ya Kunduchi, wamekuwa wakituhumu White Sand Hotel kwa kuongeza tatizo la fujo za mawimbi kutokana na hatua za kuhami maeneo yao dhidi ya mmomonyoko wa ardhi unaosabishwa na vurugu za mawimbi makubwa.

‘’Serikali ya awamu ya tano inawahitaji wawekezaji katika sekta zote za uchumi, tusingependa migogoro iendelea kwa kuwa inarudisha nyuma jitahada za serikali. Naitaka timu ya wataalum kutoka NEMC kukutana na wawekezaji hawa na kutoa suluhisho la muda mfupi huku wakijiandaa na suluhisho la kudumu katika kukabiliana na changamoto hiyo,’’ amesema Waziri Zungu.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, amewataka wawekezaji kuwaajiri maofisa wa mazingira ambao watakuwa wakifanya ‘environmental audits’ kila mwaka. Tathimini hizo zitasaidia kueleza changamoto za kimazingira kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Mzozo huu kwa kiasi kikubwa unatokana na kukosekana kwa wataalamu wa mazingira ambao wangeeleza kitaalamu katika repoti za mazingira za kila mwaka msingi wa mawimbi na uharibifu unaotokana mawimbi hayo na tatizo kushughulikiwa kwa wakati. Jitahidini kuajiri maofisa wa mazingira ambao watawasiliana moja kwa moja na NEMC kabla mambo hayajaharibika,’’ ameeleza Dk. Gwamka.

Mwanasheria wa Wellworth Hotels & Lodges Ltd, Bw. Saimon Nguka amemshukuru Waziri Zungu kwa kutembelea eneo hilo, na ameiomba serikali kuendelea kutoa ushirikiano na kufanyia kazi changamoto za kiuwekezaji.

“Tunakushukuru kwa ziara uliyoifanya na kujionea hali halisi katika fukwe hii. Tunaomba mamlaka zote za serikali kuitikia wito kwa haraka badala ya kuacha haya mambo tukayashughulikia sisi wenyewe jambo ambalo linaweza kuleta migogoro isiyo ya lazima,’’ amesema Bw. Nguka.

Ziara hiyo ya Waziri Zungu ni mwendelezo wa Wizara yake katika kushughulikia changamoto mbalimbali za kiuwekezaji hasa katika upande wa mazingira na kuhakikisha wawekezaji wanafuata kanuni na sheria za mazingira hapa nchini.

Mwisho/