NEMC yawaonya wenye viwanda kununua chuma chakavu kwa magendo
KATIKA kukabiliana biashara ya magendo ya chuma chakavu hapa nchini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wenye viwanda kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazoelekeza ununuzi wa chuma chakavu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amewaelekeza wenye viwanda kununua chuma chakavu kutoka kwa wafanyabiashara waliosajiliwa na kutambulika na Baraza.
“Utafiti wetu unaonesha uhujumu mkubwa wa miundombinu hapa nchini hali ambayo ilichangia kufunga usafirishaji wa chuma chakavu nje ya nchi.
Kuanzia sasa wenye viwanda wote watalazimika kununua chuma chakavu kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamesajiliwa na NEMC ili kulinda miundombinu,’’ alisema Dkt. Gwamaka.
Dkt. Gwamaka alisema kuwa NEMC ilishakutana na wadau na wafanyabiashara wa chuma chakavu ili kupata maoni yao yaliyotumika kutengeneza kanuni mpya za ufanyaji wa biashara ya chuma chakavu za mwaka 2019.
“Kanuni mpya zinawataka wafanyabiashara wa chuma chakavu kuwa na vibali ambavyo vitatolewa na NEMC baada ya kujiridhisha,’’ alisema na kuongeza atakaye kiuka kanuni na taratibu atachuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutaifishwa mzigo wake.
Akifafanunua zaidi kuhusu utaratibu huo, Dkt. Gwamaka alsema vibali vya kukusanya chuma chakavu vinatolewa kwa gharama ya shilingi 50,000/- tu ambapo tozo zake mwaka ni kati ya shilingi milioni na laki tano hadi milioni tano.
“Upatikanaji wa vibali vya NEMC utawagusa wafanyabiashara wote wadogo ambao wamekuwa wakikusanya tani tatu kwa mwaka na watalazimika kulipa tozo ya milioni moja na laki tano na kwa wale wanaokusanya zaidi ya tani tatu watalipia tozo ya shilingi milioni tano,’’ alisema Dkt. Gwamaka.
Alisema mbali ya kuzuia uharibifu wa miundombinu, zuio hilo liltoa nafasi ya kutafiti namna gani vyuma chakavu visafirishwe nje ya nchi pasipo kuhujumu azma ya serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.
“Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ikitekeleza azma ya kujenga uchumi wa kati na viwanda hivyo lazima NEMC iunge mkono azma hiyo kwa vitendo kwa kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa chuma chakavu kama sehemu ya malighafi muhimu kwenye viwanda,’’ alisema Dkt. Gwamaka.
Hata hivyo, Dkt. Gwamaka alisema katika kuhakikisha kuwa chuma chakavu kinapatikana kwa wingi hapa nchini, serikali inahamasisha wafanyabiashara wanaoingiza chuma chakavu kutoka nje ya nchi ambayo kila tani moja italipiwa shilingi 7,500 tofauti na wale wanaosafirisha nje watalipa shilingi 30,000/- kwa tani moja.
Hatua hizi zinazochukuliwa na NEMC zinalenga kuhakikisha miundombinu na mazingira yanaendelea kulindwa muda wote kwa manufaa na ustawi vizazi vya leo na vijavyo.
Mwisho.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15