𝐁𝐎𝐃𝐈 𝐘𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐏𝐎𝐍𝐆𝐄𝐙𝐀 𝐉𝐈𝐓𝐈𝐇𝐀𝐃𝐀 𝐙𝐀 𝐔𝐓𝐔𝐍𝐙𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐙𝐈𝐍𝐆𝐈𝐑𝐀 𝐊𝐖𝐄𝐍𝐘𝐄 𝐌𝐑𝐀𝐃𝐈 𝐖𝐀 𝐄𝐀𝐂𝐎𝐏

Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC imepongeza namna Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unavyozingatia Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira kwa kufuata matakwa yote ya Cheti Cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Profesa Esnat Chaggu alipokuwa akizungumza alipoambatana na wajumbe wa Bodi hiyo walipozuru kuona maendeleo ya Mradi huo katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga Januari 20, 2025.
Profesa Chaggu amesema kitendo Cha kupitisha bomba chini bila kuathiri chanzo Cha maji ya mto Sigi ni utaalamu wenye tija katika kuhakikisha Mazingira yetu na hasa chanzo Cha maji kinalindwa.
"Tulitamani kujua na kuona upitishaji wa bomba katika eneo la mto Sigi limefanyikaje, lakini kwa utaalamu wanaoendelea nao hakuna tatizo lolote na bomba litapita chini ya mto na maji hayataathirika kwa namna yoyote." Amesema Profesa Chaggu.
"Tumeangalia pia upande wa wataalamu wanaosimamia Shughuli zinazoendelea, tumefurahi kuona wataalamu wa Mazingira ambao ni vijana wetu waliosoma katika Vyuo vyetu na wanasimamia maendeleo ya Mradi huu mkubwa na muhimu kwa Taifa" ameongezea Profesa Chaggu.
Akizungumza kwa niaba ya wasimamizi wa Mradi huo, Mratibu wa Masuala ya Mazingira - EACOP, Bw. Joflin Bejumula amesema mradi utaendelea kusimamia taratibu zote za Utunzaji wa Mazingira kama yalivyoainishwa kwenye Cheti Cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira.
"Tunaendelea kuhakikisha kwamba matakwa yote ya Cheti Cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira yanatekelezeka na kama Mradi tumeweka utaratibu wa kutembelea maeneo ambayo Shughuli za Mradi zinaendelea na kufanya ukaguzi kubaini athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza kutokana na Shughuli tunazozifanya" Amesema Bw. Bejumula.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) litaendelea kuhakikisha kuwa Miradi yote chini inatekelezwa kwa kuzingatia Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15