JAFO AZINDUA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA


JAFO AZINDUA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amezindua maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika Kitaifa jijini Dodoma kuanzia tarehe 28 Juni hadi kufikia kilele chake tarehe 5 Juni 2022.Katika uzinduzi huo Mhe. Waziri amefanya matembezi na kushiriki katika zoezi la kupanda miti katika eneo la Iyumbu Mkoani humo.

Dkt. Jafo ametoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi kwa kushiriki kikamilifu kwenye utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali. Pia amesisitiza kuongeza juhudi za kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kila mmoja kupanda miti na kuitunza kwa maendeleo endelevu. Amezitaka taasisi mbalimbali kama shule, vyuo, hospitali, magereza na maeneo mbalimbali kupanda miti na kufanya usafi ili kudumisha usafi na uhifadhi wa mazingira.

Amesema "mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na changamoto kubwa duniani, suala la ukame maeneo mbalimbali na mvua zisizotosheleza, jambo la kufanya ni kila mwananchi kufuata ajenda ya utunzaji wa mazingira na upandaji miti ili kufikia lengo la kupanda miti millioni 276 kwa mwaka ili kuongoa mfumo ikolojia." Pamoja na hayo amewaomba wananchi kujitokeza katika viwanja vya Jakaya Kikwete katika maonesho ya maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani kuanzia tarehe 1 hadi kilele tarehe 5 ili kujifunza teknolojia mbalimbali za kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.