NEMC, BAKITA NA BAKIZA ZASHIRIKIANA KUSANIFISHA ISTILAHI ZA MAZINGIRA.


Wataalamu wa mazingira kutoka Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC wamehudhuria warsha ya kusanifisha Istilahi za Mazingira kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kuanzia tarehe 10 hadi 11 Septemba 2020.

Akiongea kwenye warsha hiyo mgeni rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt.Method Samuel amesema anawashukuru sana NEMC kwa ushirikiano walioutoa katika mchakato mzima wa usanifishaji wa Istilahi za mazingira, na iwe ni mfano kwa Taasisi zingine za Serikali na binafsi ili kulipunguzia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ugumukatika utendaji kazi wake.

“Nawapongeza sana NEMC kwa ushirikiano walioutoa kwenye mchakato mzima wa kusanifisha Istilahi za mazingira na pekee kabisa nimshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka kwa ushirikiano alioutoa mara tu baada ya kumuomba ushiriki katika kusanifisha maneno ya mazingira”.

Aidha Dkt. Method ameziomba taasisi zingine na wadau wa kiswahili watoe ushirikiano wanapoombwakushiriki katika usanifishaji wa istilahi,lengo ni kupata Kiswahili sanifu na kinachokidhi mahitaji ya wadau katika sekta mbali mbali na ndiyo jukumu la BAKITA.

“Nawaomba wadau na taasisi zingine zitoe ushirikiano pale tunapohitaji Istilahi, lengo ni kupata Kiswahili sanifu na kinachokidhi mahitaji ya wadau katika sekta mbali mbali na ndiyo jukumu letuBAKITA. Tusipopata ushirikiano wa kutosha madhara yake ni kutumia lugha isiyo sanifu na hili bado ni tatizo kubwa sana hapa nchini.

Hali kadhalika Bi Consolatha Mushi Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) amesema kuwa, pamoja na usanifishaji wa istilahi za Nyanja mbali mbali kufanyika, badohaitoshi ni lazima sasa Baraza la Kiswahilikuchukua jukumu la kusanifisha istilahi za mazingira kwasababu zinamgusa moja kwa moja mwananchi katika maisha yake ya kila siku na ni suala mtambuka.

“Mazingira ni suala mtambuka linayagusa moja kwa moja maisha ya mwanadamu hivyo tuliona ni vyema matumizi ya lugha ya Kiswahili yawe sanifu katika eneo hili, na ndiyo maana tumewashirikisha wataalamu wa mazingira kutoka NEMC kuleta istilahi sambamba na kuwaalikawabobezi wa lugha ya Kiswahili kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya shughuli hii.”

Naye Bi Angela Kileo, Afisa sheria Mkuu kutoka NEMC amesema Sheria, sera na kanuni za mazingira nyingi zipo katika lugha ya Kiingereza hivyo inalazimu kusanifuistilahi ili zitumike kwa lugha yetu ya Kiswahili. Hii itasaidia kufikisha ujumbe kwa urahisi kwenye jamii katika masuala yote yanayohusu mazingira kwasababu ni lugha yetu ya Taifa na ndiyo inayotumiwa na Watanzania ni katika mawasiliano.

“Sheria, sera na kanuni nyingi za mazingira zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza na lugha yetu Watanzania ni Kiswahili hivyo tumeona ni vyema kupata maneno ya Kiswahili ambayo yalikuwa hayapo hapo awali badala yake yalikuwa yakitumika maneno ya Kiingereza peke yake”.