HATUA ZA KUFUATA WAKATI WA KUFANYA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA NA JAMII (TAM)
1. MFUMO WA USAJILI MTANDAONI
Baraza kwa sasa linasimamia miradi inayofanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) kwa njia ya kielektroniki kupitia usajili wa mtandaoni (http://eia.nemc.or.tz) njia hii inamuwezesha mwekezaji kuanzisha mchakato wa TAM au Ukaguzi wa Mazingira (EA) kupitia mfumo wa usiamizi wa miradi (PMS)
i) Malengo ya Usajili wa Mtandaoni
· Kuongeza ufanisi katika mchakato wa TAM/Ukaguzi wa mazingira kwa kuokoa gharama na wakati kwa pande zote zinazohusika
· Unamwezesha mwekezaji kufuatilia kwa urahisi maendeleo ya mradi
· Unawezesha upatikanaji na utunzaji wa taarifa za TAM sehemu moja
ii) Zifuatazo ni hatua zinazopaswa kufuatwa wakati wa usajili wa miradi kwa njia ya mitandao
Hatua ya kwanza ni:
Usajili (Registration): Mwekezaji hujaza fomu ya usajili kwa njia ya mtandao, kutuma muhtasari wa mradi (kwa mIradi ya kundi B2), taarifa ya Mawanda na hadidu za rejea za mradi (kwa miradi ya kundi A), Muhtasari na hadidu za rejea za mradi (kwa miradi inayofanya ukaguzi wa mazingira) na kulipa ada ya usajili.
Hatua ya pili ni:
Tathmini ya Athari kwa mazingira: Mwekezaji kwa kushirikiana na Mtaalam mwelekezi wa Mazingira anakusanya taarifa za awali (baseline data) za mradi, anafanya tathmini ya madhara na namna bora ya kuzuia madhara na kuandaa taarifa ya TAM/taarifa ya ukaguzi wa Mazingira (EA) na kuituma kwenye mfumo wa kielektroniki. Mwekezaji pia atalipia gharama ya kupitia taarifa ya TAM/taarifa ya ukaguzi wa mazingira kupitia PMS.
Hatua ya tatu ni:
Mapitio ya taarifa za mradi (Review): Baraza litatembelea eneo la mradi husika kwa kushirikiana na wadau wa mradi na kupata maoni yao. Hii hufuatiwa na kikao cha kamati ya wataalam (Technical Advisory Committee meeting) kwa ajili ya kulishauri Baraza.
Hatua ya nne ni:
Mapendekezo ya kikao cha Kamati ya wataalam: Baraza linaweka pamoja maoni ya kikao cha wataalam na kuyatuma kwa mwekezaji ili aweze kuboresha taarifa ya TAM/taarifa ya ukaguzi wa Mazingira na kisha kutuma taarifa hiyo kwenye mfumo.
Hatua ya tano ni:
kuwasilisha mapendekezo ya mradi kwa Mh. Waziri wa Mazingira: Mwekezaji atatuma Muhtasari wa Mradi/taarifa ya TAM/Taarifa ya ukaguzi wa Mazingira iliyoboreshwa kwa Baraza na kama Baraza litaridhishwa na taarifa hiyo, Baraza litatuma mapendekezo hayo ya mradi kwa Waziri wa Mazingira kwa ajili ya kuidhinisha na kutoa cheti kwa mradi.
Hatua ya sita ni:
Kuidhinishwa kwa Muhtasari wa mradi/taarifa ya TAM/Ukaguzi wa mazingira: Baada ya kusainiwa kwa cheti na Waziri, kitarejeshwa NEMC kwa ajili ya kukabidhiwa kwa mwekezaji. Waziri anaweza kuidhinisha au kutoidhinisha Muhtasari wa mradi/taarifa ya TAM/ukaguzi wa mazingira ndani ya siku 30 kulingana na Sehemu ya 92(1) ya EMA Cap. 191.