Utangulizi
KIKOSI KAZI CHA TAIFA CHA MIAMBA YA MATUMBAWE
‘TANZANIA CORAL REEF TASK FORCE (TzCRTF)’
1.0 UTANGULIZI
Kikosi kazi cha miamba ya matumbawe Tanzania (Tanzania Coral Reef Task Force - TzCRTF) kiliundwa baada ya kikosi kazi cha matumbawe cha ukanda wa magharibi ya Bahari ya Hindi (Western Indian Ocean Coral Reef Task Force - WIO CRTF) kilichoanzishwa mwaka 2002 na kupitishwa kwa maamuzi ya mkutano wa nchi wanachama (CoP 3/2) kuhusu uhifadhi na utunzaji wa matumbawe na mifumo ikolojia inayohusiana na Mkataba wa Nairobi, uliofanyika Antananarivo, Madagaska mwaka 2004.
Aidha, Nchi wanachama za Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika zikiwemo Kenya, Msumbiji, Somalia, Afrika Kusini, Tanzania, na Nchi za Visiwa vya Comoro, Madagaska, Mauritius, Reunion, na Ushelisheli ‘Seychelles’ zimetia saini Mkataba huo uliobainisha haja ya kuimarisha uwezo wa kuratibu maeneo maalum kupitia uanzishwaji wa vikosi kazi. Kwa hiyo, Kikosi kazi cha miamba ya matumbawe nchini kinaendana na ahadi ambazo ziko chini ya mkataba huu.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutokana na mamlaka yake katika kusimamia mazingira, lina jukumu la moja kwa moja la kuratibu shughuli za kikosi kazi hiki nchini. Kikosi kazi cha Ukanda wa magharibi ya Bahari ya Hindi cha Matumbawe kilianzishwa kama kituo cha ushauri kwa masuala yote yanayohusu utafiti wa miamba ya matumbawe, ufuatiliaji, uhifadhi na usimamizi.
Hivyo basi kikosi kazi hiki kinaitishwa na kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC na sekretarieti iliwekwa NEMC ili kushughulikia majukumu na mahitaji ya kitaifa na utawala. Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni msimamizi na mratibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Nairobi, ina jukumu la kujenga uwezo na kusimamia kwa ujumla kazi za Kikosi Kazi. Wakati huo huo, Taasisi ya Sayansi ya Bahari (IMS) iliyoko Zanzibar na ambayo ni kituo cha Ubora cha utafiti na ufuatiliaji wa miamba ya matumbawe, ina jukumu la kushughulikia masuala ya kukusanya taarifa za kisayansi na kufanya ufuatiliaji.
Kikosi kazi hiki kinaundwa na wajumbe kutoka Taasisi za Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayohusika na usimamizi wa rasilimali za pwani na bahari nchini Tanzania (Bara na Zanzibar). Kikosi Kazi hukutana angalau mara mbili kwa mwaka ili kujadili masuala kuhusu miamba ya matumbawe na pia kuandaa na kutoa ripoti ya hali halisi ya miamba hiyo.
Kazi kuu ya Kikosi kazi hiki ni kuratibu shughuli zinazoshughulikia utekelezaji wa maamuzi yanayohusiana na miamba ya matumbawe na mifumo ikolojia inayohusika. Kwa kufanya hivyo, Kikosi kasi kinatoa msingi wa kisayansi ambapo maamuzi sahihi juu ya utafiti na usimamizi wa miamba ya matumbawe unapaswa kufanywa. Pia ina jukumu la kuongoza sekretarieti ya wapangaji mipango na wasimamizi wa kitaifa kuhusu masuala yote yanayohusiana na miamba ya matumbawe na mifumo ikolojia iliyopo. Hivyo ni kiungo kati ya sekta za serikali, na uimarisha usimamizi endelevu wa mazingira ya bahari na pwani. Kikosi kazi hiki pia kinatoa fursa katika kushughulikia kwa pamoja masuala ya pwani ambayo hayawezi kutatuliwa na sekta moja bali kwa ushirikiano wa pamoja.