WAZIRI JAFO ATEMBELEA KIWANDA CHA TWIGA CEMENT


WAZIRI JAFO AFANYA ZIARA KATIKA KIWANDA CHA TWIGA CEMENT.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mhe.Dkt Selemani Jafo amevitaka viwanda vyote Nchini kuiga mfano wa kiwanda cha Twiga Cement kilichopo Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam kwa kutunza na kuhifadhi mazingira.

Aliyasema hayo leo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa kiwanda hicho cha sementi ambacho kinatumia nishati ya gesi katika uzalishaji wa sementi pamoja na kuanzisha mpango wa kukusanya taka za aina mbalimbali kutoka katika dampo la Pugu Kinyamwezi na maeneo mengine na kuzalisha nishati ya gesi.

“Twiga sementi ni kiwanda cha mfano wa kuigwa kwani ni kiwanda cha kwanza kuzalisha sementi kwa kutumia nishati ya gesi pamoja na kukusanya taka na kuzichakata kuwa nishati”

Akiwa Kiwandani hapo Mheshimiwa Jafo ametembelea mtambo wa kisasa utakaotumika kuteketeza mifuko ya plastiki iliyokusanywa wakati huu wa kampeni ya kukamata mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na kupongeza Mkoa wa Dar es salaam kwa kufanikiwa katika suala zima la usimamizi wa katazo la mifuko ya plastiki.

“Niwapongeze sana Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanikiwa katika kampeni hii ya kukamata mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na pia niwashukuru Twiga Cement kwa kukubali kutumia mitambo yao kuteketeza mifuko hiyo”

Katika ziara hiyo Waziri Jafo alipanda mti katika kitalu cha miti cha Kiwanda hiko kama ishara ya kuonesha umuhimu wa upandaji miti na kusisitiza jamii kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kupanda miti kila siku.

“Niwapongeze sana kwa juhudi zenu katika utunzaji wa mazingira kwa kuanzisha kitalu hiki cha miti ambapo kwa sasa tuko kwenye kampeni muhimu ya kupanda miti mmeonyesha kitu kikubwa sana”.

Naye Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Ufuatiliaji wa Sheria ya Mazingira kutoka NEMC Injinia Redempta Samuel amekipongeza kiwanda cha Twiga sementi kwa kukubali kuteketeza mifuko ya plastiki kwa kutumia mitambo yao lakini pia kwa kuchakata taka na kuzalisha nishati ya gesi.

“ Nitoe wito kwa Wananchi kutengenisha taka toka zinapozalishwa majumbani ili iwe rahisi zinapokuja kwenye kiwanda hikiziweze kuchakatwa kwa urahisi na kuzalisha nishati mbadala, tujitahidi tusichanganye takataka kwa sababu kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha takataka zote ngumu, iwe ni plastiki,mabaki ya mbao, mabaki ya pumba za mpunga na mabaki ya maganda ya korosho.”

Katika hatua nyingine Mhe Jafo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuandaa tuzo maalumu ya Waziri wa Mazingira kwa kiwanda cha Twiga Cement kwa kutunza na kuhifadhi mazingira kutokana na kuendesha shughuli zake kwa kutumia nishati ya gesi lakini pia kwa kuja na mpango wa kukusanya taka, kuzichakata na kuzalisha nishati ya gesi na tuzo nyingine kwa kijana aliyeko Mkoani Mwanza anayetengeneza mabegi ya wanafunzi ya shule kwa tumia mifuko ya sementi iliyotumika