WAZIRI JAFO AIPONGEZA WIZARA YA ELIMU KWA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA KATAZO LA MATUMIZI YA KUNI NA MKAA KWA TAASISI ZA UMMA ZINAZOLISHA WATU ZAIDI YA 100.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameipongeza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kuwa kinara wa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais juu ya katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma zinazoandaa na kulisha watu zaidi ya mia moja (100) kwa siku, kuanzia Januari, 2024.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari februari 20, 2024 katika ofisi za Makao makuu ya NEMC Jijini Dodoma na kutoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali yahusuyo usitishaji wa matumizi ya kuni na makaa kwa Taasisi za Umma na kubainisha Wizara hiyo kupitia taasisi zake kuwa imetekeleza kwa zaidi ya asilimia 85.
“Katika utekelezaji wa agizo hili serikali napenda kuipongeza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kuwa kinara kwa taasisi zake nyingi kutekeleza agizo hili la serikali kwa zaidi ya asilimia 85. Taasisi zingine zinapaswa kuiga mfano mzuri uliofanywa na Wizara ya Elimu na Taasisi zake.” Amesema Waziri Jafo.
Amesema lengo la maelekezo hay ani kupunguza madhara ya kiafya na Mazingira yanayosababishwa na kukithiri kwa matumizi ya Kuni na Mkaa katika jamii zetu na ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya kupikia.
Dkt. Jafo amesisitiza kuwa katazo hili haliwahusu watumiaji katika ngazi ya Kaya na watumiaji wadogo bali limeanza kwa watumiaji wakubwa. Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waanze kutumia nishati safi ya Kupikia.
“Kama nilovosema, hap awali, katazo hili linazihusu Taasisi kubwa, Taasisi hizo ziko chini ya TAMISEMI, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalumu, Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia Pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi” Amesema Dkt Jafo.
Dkt Jafo amesema Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 inahimiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi Mazingira ikiwemo rasilimali za misitu, hivyo ili kufikia lengo hilo, sera inahamasisha matumizi ya nishati mbadala wa kuni na mkaa kwa lengo la kupunguza ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta ipo kwenye maandalizi ya kuunda timu ya Wataalam itakayoweza kutembelea taasisi husika ili kufuatilia hatua zinazoendelea katika utekelezaji wa katazo hilo na kutoa ushauri wa kitaalam.
Itakumbukwa kuwa tarehe 01 Novemba, 2022, Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia. Katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo ya kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya mia moja (100) kwa siku, ifikapo Januari, 2024. Lengo la maelekezo hayo ni kupunguza madhara ya kiafya na mazingira yanayosababishwa na kukithiri kwa matumizi ya kuni na mkaa katika jamii zetu.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15