WAZIRI JAFO AIAGA NEMC RASMI, AISHUKURU KWA USHIRIKIANO ILIOMPATIA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) ameagana na watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Julai 22,2024 katika Ofisi za NEMC Dar es salaam.
Hafla hiyo ni kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo Waziri Jafo amebadilishana nafasi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Dkt.Ashatu Kijaji.
Waziri Jafo alipozungumza katika hafla hiyo ya kuagana amewashukuru watumishi wote wa Baraza kwa kutoa ushirikiano kipindi chote alichokuwa akihudumia kwa nafasi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ikiwa ni pamoja na kazi nzuri wanaoyoifanya ya kusimamia Uhifadhi wa Mazingira na miradi zaidi ya elfu 9 inayolenga kuleta maendeleo Nchini.
“Ndugu zangu niwapongeze na ninajivunia kufanya kazi nanyi kwa kipindi chote nilichokuwa hapa, uwekezaji wa miradi karibu elf 9 imesajiliwa na huu ni uwekezaji mkubwa sana na mikono yenu ndio inashughulikia miradi hiyo. Niwapongeze kwa kusimamia miradi hii kwa kasi kubwa na kutekeleza majukumu yenu” amesema Waziri Jafo.
Waziri Jafo pia ametoa wito kwa watumishi kushirikiana na Waziri Dkt.Ashatu Kijaji katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali hasa masuala mazima ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipozungumza amempongeza Waziri Jafo kwa kazi kubwa aliyoifanya ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi inayolenga kutunza Mazingira kama mradi wa kudhibiti matumizi ya Zebaki, kusimamia utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki na sauti zilizozidi viwango.
Julai 2,2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alimteua Dkt. Selemani Jafo (mb) kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara akitokea Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akibadilishana na Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akitokea Wizara ya Viwanda na Biashara.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15