NEMC YAZITAKA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA KOTE NCHINI KUONA FURSA ZILIZOPO KATIKA TAKA NGUMU.


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeyataka majiji, Halmashauri za Miji na Manispaa kuona na kutambua fursa za ajira zilizopo katika taka ngumu na kuweka mikakati wezeshi ya kufanikisha hilo ili kutunza Mazingira.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi wakati akifungua mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na NEMC na Kituo cha Sayansi ya Mazingira (CSE) cha nchini India kuhusu udhibiti wa taka ngumu.

Amesema taka ngumu ni fursa wezeshi ya ajira kwa vijana hasa ikitumiwa kutengeneza nishati na bidhaa mbalimbali hali itakayoweka mazingira katika usafi.

Ameongeza kuwa upo umuhimu wa kukusanya takwimu ya taka zinazozalishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini na namna zinavyotunzwa ili ziwe fursa kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali hasa ikizingatiwa kituo Cha Sayansi Cha India (CSE) tayari kimesha andaa mwongozo wa namna ya kuzitumia taka hizo kama rasilimali.

“Taka ngumu kwenye manispaa zetu Tanzania zinaendelea kuongezeka kutokana na wingi wa watu na shughuli za binadamu, kwa hiyo tunapaswa kuangalia namna ya kutumia taka ngumu hizi kama fursa na tukifanikiwa kwenye hili tutayaweka mazingira yetu safi,” amesema Dkt Immaculate Sware

Naye Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira (NEMC), Dk. Menan Jangu alipozungumza alisema upo umuhimu wa kuboresha mifumo ya udhibiti wa taka ngumu ambazo zimekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira nchini kwani Serikali kwa kushirikiana na wadau na kituo Cha CSE India tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha taka ngumu zinakuwa fursa.

Mkutano huo umewashirikisha maofisa kutoka Manispaa na Majiji, kwenye Mikoa sita ya Dar es salaam, Arusha, Mbeya, Dodoma, Mwanza na Tanga kwa lengo la kuwajengea uelewa na mikakati ya kusimamia ya takangumu kwenye maeneo yao.