NEMC YAWAONYA WANANCHI WANAOTAPISHA VYOO KIPINDI CHA MVUA


Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewaonya wananchi wote wenye tabia za kutapisha vyoo vyao hasa katika kipindi cha mvua na kuwataka waache tabia hiyo ili kuilinda jamii dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza leo hii Mkurugenzi wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wananchi wote watakaobainika kufanya kitendo hicho.

“Hatutakuwa na msamaha na watu wanaotapisha vyoo wakati wa mvua. Tumekuwa tukifaidi uzingatiaji wa sheria kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, ndio maana hujasikia kipindupindu. Sasa tukianza kusikia kipindupindu sasa huyo mtu hatutamuonea huruma kwa maana anataka kuturudisha nyuma” amesema Dkt. Gwamaka.

Dkt. Gwamaka ameongeza kuwa jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za wote wenye tabia ya kutapisha vyoo vyao kipindi cha mvua na kutokuwaachia NEMC pekee kufuatilia maeneo hayo.

“Wananchi wa maeneo husika wasiwategemee maafisa wa Mazingira pekee. Wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa NEMC watakapobaini kuna mwananchi ambaye anatapisha choo chake kipindi cha mvua. Kikosi chetu cha dharura kitafika mapema na kuweza kuwawajibisha” ameeleza Dkt. Gwamaka.

Kutokana na Tanzania kuingia katika uchumi wa kati Dkt. Gwamaka amesema kuwa ni vyema wananchi kuhakikisha wanaenda kwa kasi hiyo ili kuzuia kutokea kwa magonjwa ya mlipuko itakayorudisha taifa nyuma.

“Tumekwisha kuwa nchi ya uchumi wa kati. Kwahiyo mtu asitake kuturudisha kwenye uchumi wa chini. Tumeshakuwa wastaarabu, tumeshakuwa waelewa. Sasa badala ya kutapisha choo ona maafisa Mazingira wa Mtaa au Kata kuona namna gani ambavyo unaweza kupakua choo chako. Magari yako mengi na mnaweza kuchanga watu watatu gari ikaja na kunyonya uchafu. Sasa ukisubiri wakati wa mvua ndio utapishe sisi hatutakuonea huruma” amesisitiza Dkt. Gwamaka

Hatahivyo NEMC imeendelea kusimamia Mazingira kwa kutoa elimu na kuhakikisha usalama unakuwepo katika jamii zetu. Katika kipindi hiki cha mvua Baraza limeendelea kuwaasa wananchi kutunza na kulinda Mazingira kwa ustawi wa afya za kizazi cha sasa na cha baadae.