​NEMC YATOA SIKU SABA KWA KAMPUNI YA CHANZI LIMITED ARUSHA KUDHIBITI UCHAFUZI WA MAZINGIRA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa siku saba kwa Kampuni ya Chanzi Limited inayojishughulisha na uzalishaji wa funza kwa ajili ya utengenezaji wa Chakula cha mifugo, kuhakikisha wanazuia harufu kali inayotokana na shughuli zinazofanyika kiwandani hapo ili kuondoa kero kwa wananchi na kulinda Mazingira

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria - NEMC Dkt. Thobias Mwesiga Richard alipozuru eneo la tukio na kubaini ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira hali iliyosababisha uharibifu wa hali ya hewa na kuleta kero kwa wananchi.

“Tumefanya ukaguzi katika eneo hili na tumejiridhisha kwamba kweli changamoto hiyo ipo, na changamoto yenyewe ni harufu kali inayotoka hapa ambayo inawaathiri wakazi wa maeneo haya na sisi maelekezo yetu kama Baraza ni kwamba kwanza kiwanda hiki kihamishiwe eneo lingine mbali na makazi ya wananchi, eneo ambapo hakitakuwa karibu na wananchi” Amesema Dkt. Thobias.

Aidha Dkt. Mwesiga amemtaka Mwekezaji kuhakikisha anadhibiti harufu hiyo mbaya kwa haraka wakati akiendelea kufuatilia kukamilika kwa mchakato utakaomuwezesha kuhamisha kiwanda chake eneo la makazi ili kuwaondolea kero wananchi na kulinda mazingira.

Naye Bi. Mayasa ambaye ni Meneja wa Kampuni ya Chanzi limited alipozungumza amekiri kuwepo kwa kero hiyo na kuahidi kutekeleza agizo hilo kwa wakati ili kunusuru afya za raia wa eneo hilo na kulinda Mazingira.