​NEMC YATOA ELIMU YA UDHIBITI WA MATUMIZI YA ZEBAKI KATIKA KONGAMANO LA WANAWAKE WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo (EHPMP) limeshiriki Kongamano la Wanawake Wachimbaji Wadogo Mkoani Geita ikiwa ni muendelezo wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika Machi 9,2024.

NEMC imewakilishwa na Mratibu wa Mradi huo Mhandisi Dkt. Befrina Igulu ambapo ametumia jukwaa hilo kuzungumza na Wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu mkoani Geita na kuelezea nia ya Serikali kuwa na Mpango wa kupunguza na hatimae kuondoa kabisa matumizi ya Zebaki katika kuchenjua dhahabu kutokana na Zebaki kuwa na athari nyingi kiafya na kimazingira.

"Kemikali inayotumika na Wachimbaji ambao mitaji yao ni midogo na hasa wanawake ni Zebaki na ni moja ya kemikali zenye athari kubwa za kiafya na kimazingira, tumewapa thamani ya kipekee wanawake kwa sababu tabia ya kemikali yanyewe ya Zebaki ni kwamba inabebwa kutoka kiumbe kimoja kwenda kingine kwaiyo ikiingia kwa mama aliyefika umri wa kushika mimba madhara yake yatahamia kwa mtoto na kusababisha madhara kiafya" Amesema Dkt. Befrina.

"Madhara yake ni pamoja na mimba kutoka, mtoto kuzaliwa na uelewa hafifu jambo ambalo linaharibu ustawi wa jamii kiujumla, kama Serikali ni nia yetu ya dhati tupunguze na ikiwezekana kuacha kabisa matumizi ya Zebaki" Ameongezea Dkt. Befrina.

NEMC inatekeleza Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kufuatia makubaliano ya kidunia ya kuondoa kabisa matumizi ya Zebaki hadi kufikia mwaka 2030 hivyo Serikali imedhamiria kutoa elimu kwa Wachimbaji wadogo ili waanze kuendana na matumizi ya njia mbadala za uchenjuaji wa dhahabu