NEMC YASHIRIKI MBIO ZA KUHAMASISHA UTUNZAJI WA FUKWE ZA BAHARI


NEMC yashiriki katika mbio (marathon) zilizofanyika Rongoni beach, Kigamboni, jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zimeandaliwa na kampuni ya Dar Beach Marathon International kwa lengo la kuhamasisha jamii katika kutunza fukwe za Bahari.

Kampuni hio ambayo imeanzishwa mwaka 2019 kwa lengo la kusafisha fukwe za Bahari, huwa inafanya usafi huo mara kwa mara kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni na Vikundi mbalimbali vya kijamii.

Kutokana na Kampuni hiyo kushiriki katika kusafisha maeneo ya fukwe za bahari, iliamua kuandaa mbio ambazo zitahamasisha jamii nzima na wadau katika kutunza mazingira hayo, kauli Mbiu ikiwa “Kimbia, tunza mazingira ya fukwe.”

Aidha Bw. Faki Matauka ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Kampuni hiyo ameeleza kuwa “hii ni mara ya pili kwa Kampuni kuandaa mbio ambazo zinahamasisha jamii kutunza fukwe za Baharina kwa kiasi fulani tumefanikiwa kuhamasisha jamii hasa kwa upande wa Kigamboni katika kutunza mazingira ya fukwe. Pia tunaziomba kampuni za kutunza mazingira zishirikiane nasi mwakani katika kufanikisha azima hiyo”

Aliendelea kueleza kuwa wamefurahishwa na NEMC kushiriki kikamilifu katika mbio hizo kwani ndio wadau wakubwa katika kuhifadhi na kusimamia mazingira kitaifa. “

NEMC ilishiriki katika mbio hizo ili kuhamasisha juhudi za Taasisi zisizo za Kiserikali na jamii kwa ujumla kutunza mazingira na kuhakikisha yapo safi na salama kwa ajili ya ustawi wa viumbe vyote vya baharini na nchi kavu.