​NEMC YANOA WAANDISHI WA HABARI -ELIMU YA MAZINGIRA.


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendesha semina ya siku moja ya elimu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa vyombo vya habari.

Semina hiyo iliyohusisha vyombo vya habari takribani 15 na mada 4 za mazingira kuwasilishwa imefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Baraza uliopo jijini Dara es salaam.

Akifungua semina hiyo Mkurugenzi wa utawala na fedha Bw Dickson Mjinja kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa NEMC amesema lengo ni kuwajengea uwezo waandishi hao ili waweze kuwa mabalozi wazuri katika utekelezaji wa majukumu yao ya habari hususani za mazingira.

Amesema Mazingira ni jambo mtambuka hali inayomlazimu kila mmoja wetu kuwajibika katika kuyatunza na kuyahifadhi kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Mada zilizojadiliwa ni pamoja na Usimamizi wa Mazingira Tanzania, Umuhimu wa ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM), Katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na taka ngumu, pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira sura "191".

Waliowasilisha mada kutoka Baraza la Mazingira ni Bw.Anold Mapinduzi Meneja wa NEMC Kanda ya Temeke, Bw Jamal Baruti Meneja wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM), Hamad Taimur Kaimu Mkurugenzi kutoka kurugenzi ya uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria (DECE), pamoja na Bw.Onesmo Ndinga kutoka kurugenzi ya Sheria (DLS)

Vyombo vya habari vilivyoshiriki ni TBC, Chanel Ten, Star Tv, Clouds TV, ITV, Jamii forums, The Guardian/Nipashe, Kiss FM, Radio One, Wasafi, TV E, Mwananchi, pamoja na Daily news/Habarileo.

Akiwasilisha mada ya usimamizi wa Mazingira Tanzania, Meneja wa NEMC Kanda ya Temeke Bw.Anold Mapinduzi alisema Mazingira ni uhai endelevu wa binadamu na endapo kutatokea kusigana kwa Sheria kuhusu masuala ya Mazingira, itakayosimama ni Sheria ya Mazingira.