​NEMC KUSHIRIKIANA NA PEW NA WETLANDS INTERNATIONAL KATIKA UHIFADHI WA MAENEO YA FUKWE ZA BAHARI


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali ya Pew Charitable Trusts (PEW) na Wetlands International (WI) wajipanga kuhifadhi maeneo ya fukwe za bahari.

Hayo yamebainishwa Aprili 17,2024 katika mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira ) Dkt. Selemani Jafo na Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimataifa yasiyo ya Kiserikali ya The Pew Charitable Trusts (PEW) Ndg. Simon Redds na Wetlands International (WI) Bi. Julie Mulonga pamoja na timu ya wataalamu walioambatana nao kwa lengo la kuanisha fursa zilizopo kwenye uhifadhi wa maeneo ya fukwe za bahari ikiwa ni pamoja na mifumo ya ikolojia ya mikoko na nyasi bahari (sea grass) kwa faida za kutunza bionuai na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Waziri Jafo alipozungumza ameshukuru na kueleza utayari wa Serikali katika kushirikiana nao na kubainisha kuwa taarifa za kitafiti zitakazotokana na mradi huo zitasaidia katika maandalizi ya taarifa ya nchi kuhusu mchango wa kitaifa wa kupunguza viwango vya gesi joto duniani.

Mkutano huo umefanyika katika Ofisi za Baraza jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC Dkt. Menan Jangu na wataalamu wa Baraza.