NAIBU KATIBU MKUU KILIMO AIPONGEZA NEMC KUSHIRIKI MAONESHO YA NANENANE


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Mohamed Omar azuru banda la NEMC Maonesho ya Nanenane yenye kaulimbiu isemayo " chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi" yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Akiwa bandani hapo amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa ushiriki wa maonesho haya kwani ndio sekta muhimu katika kukuza uchumi wa kati wa viwanda kwa kuhimiza masuala mazima ya Uhifadhi na Usimamizi wake kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika sekta zenye sifa za kutoa ajira nyingi, zinazotoa kipato kwa wananchi na zinazochangia malighafi za uzalishaji viwandani kama vile sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa maendeleo endelevu ya Mazingira na Uchumi.