Kamati ya Bunge yaridhishwa utunzaji mzaingia mradi reli ya kisasa


Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Bw.Suleiman Saddiq(MB) aliyasema hayo walipotembelea mradi huo eneo la Pugu kujionea jinsi unavyoendelea na namna sheria zinavyofatwa katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira

kipindi chote cha utekelezaji cha mradi. "Mradi huu ni mkubwa kwa nchi hivyo ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na ufatiliaji wa karibu wa maendeleo ya mradi sambamba na utunzaji wa mazingira," alisema Bw.Saddiq.

Alisema Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lishirikiane kikamilifu na wadau wengine katika mradi wa SGR kuhakikisha mazingira yanalindwa ili mradi utakapo kamilika athari za kimazingira zisiwepo na kuufanya mradi uishi kwa muda mrefu.

"Elimu kwa wananchi wanaoishi kando ya mradi iendelee kutolewa iliwaelewe faida za mradi na pia athari zinaweza kutokana na mwingiliano wa watu jambo ambalo litawasaidia kujilinda na pia kufaidika kupitia fursa zitokanazo na mradi,"alisema Bw.Saddiq.

Alisema miradi kama hii ishirikishe jamii ili iweze kufaidika kupitia fursa za mradi huo na sehemu ya fedha ya mradi iweze kufanya maendeleo katika maeneo ambayo mradi huo wa SGR unapita na kuwafanya wananchi waweze kupiga hatua kimaendeleo.

"Serikali imetoa kiasi kikubwa cha fedha kufanikisha mradi huu hivyo ili kwenda sambamba na thamani ya fedha ni muhimu kuhakikisha maendeleo ya mradi yanakwenda sawa na utunzaji na uhifadhi wa mazingira,"alisema.

Bw.Saddiq alishauri kuwepo kwa kitengo maalum cha mazingira katika mradi wa SGR ili kufanya ukaguzi na usimamizi endelevu wa mradi jambo litakalosaidia kulinda mazingira na kuufanya mradi kuwa endelevu.

Katika hatua nyingine Bw.Saddiq alipongeza hatua zinazochukuliwa na Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) kwa kuhakikisha miundombinu ya nishati inaboreshwa na pia upatikanaji wa umeme unakuwa wa uhakika jambo linalotoa uhakika kuwa mradi wa SGR hautakwamishwa kwa sababu ya nishati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt.Samuel Gwamaka alisema amepokea mapendekezo na maagizo ya kamati na kuahidi watayafanyia kazi ili kuhakikisha mazingira yanalindwa ili kuufanya mradi kuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na baadaye.

"Jukumu letu NEMC ni kufanya ufatiliaji wa namna mradi unavyokwenda na usimamizi wa mazingira unavyozingatia na wakandarazi kulingana na cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira(EIA)," alisema Dkt.Gwamaka

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania( TRC), Bw.Masanja Kadogosa alishukuru kamati ya bunge kutembelea na kujionea mradi unavyoendelea na pia alisema mapendekezo yaliyotolewa na kamati watayazingatia ili kuboresha utendaji kazi na miundombinu iweze kuwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Ziara ya siku moja ya Kamati ya kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira ilitembelea eneo la mradi wa SGR pugu na Kinyerezi katika mradi wa umeme kujionea hali ya miradi ilivyo sambamba na utunzaji wa mazingira.

Mwisho.