​Waziri Sima: NEMC haitakuwa kikwazo kwa wawekezaji


NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Bw. Mussa Sima amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) ambalo lipo chini ya Ofisi yake kwa namna
linavyopambana kuweka mazingira rafiki ili kuendelea kuwavutia
wawekezaji hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara yake mkoani Mtwara,
Bw. Sima amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo, ofisi yake
imeendelea kufanyia kazi mabadiliko mbalimbali ya kanuni na sheria ili
kwenda sambasamba na azma ya serikali ya ujenzi wa uchumi wa kati na
viwanda pasipo kuathiri mazingira.
“Tunapozungumzia mazingira tunazungumzia juu ya uhai wetu, hivyo kama
Wizara yenye jukumu la kusimamia mazingira tunalazimika kusimamia
ustawi wa jamii bila kuathiri uwekezaji,” alisema Bw. Sima
Bw. Sima amesema kuwa tayari ofisi yake imechukua hatua kadhaa ikiwemo
kurekebisha baadhi ya tozo hali ambayo imepunguza malalamiko
mengikutoka kwa wawekezaji.
‘’Huko nyuma tulikuwa tukitoza asilimia moja ya jumla ya mradi au
biashara lakini sasa tumeganya miradi ambapo kila mradi utakuwa na
tozo yake. Mfano huko nyuma wamiliki wa visima vya mafuta walikuwa
wanatozwa mpaka milioni 10 lakini kwa marekebisho ya sasa watakuwa na
tozo ya milioni 4,’’ alisema Bw. Sima.
Sima aliongeza changamoto nyingine kuwa ni uchelewashaji wa Tathmini
ya Athari kwa Mazingira (EIA) ambapo ilikuwa inachukuwa siku 149
lakini kwa marekebesho ya kanuni yaliyofanywa mwezi Septemba, 2018
yalipunguza siku hizo na kuwa 95 tu.
“EIA ilikuwa inachukua muda mrefu sana na badaa ya kutafakari kwa
kina, tuliamua kufanya mabadiliko ya kanuni ambapo tumetoka siku 149
na sasa zimekuwa siku 95 hali ambayo inaonyesha ni kwa namna gani
tumelenga kurahisisha uwekezaji,’’ alifafanua Bw. Sima na kuongeza
“Tatizo la ucheleweshwaji wa EIA sio tatizo la NEMC bali ni la
Wataalamu Elekezi ambao wamekuwa na namna yao katika utekelezaji wa
miradi, hata hivyo tumeshakutana na tumeweka utaratibu wa tozo ambao
unawiana na ule wa serikali,”
Aidha alitumia nafasi hiyo kueleza mchango wa Wakaguzi wa Mazingira
ambao wapo kila mkoa kwa namna wanavyofanya kazi nzuri lakini hawawezi
kufanya nje ya utaratibu za mikoa.
“Natoa rai kwa wakaguzi wa mazingira kote nchini kutengeneza mpango
kazi na kuukabidhi ofisi ya mkoa ili watambulike wanafanya kazi gani
kwani hawa ni wadau muhimu sana katika mazingira na tuliwatumia wakati
wa utekelezaji wa katazo la ututumiaji wa mifuko ya plastiki,” alisema
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kupitia Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wameendelea kuchukua
hatua madhubuti katika kuhakikisha utekelezaji wa azma ya serikali ya
uchumi wa viwanda inatekelezeka pasipo kuathiri mazingira.