​JAFO AIPONGEZA NEMC KWA USIMAMIZI WA SHERIA YA MAZINGIRA MRADI WA JNHPP


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe Dkt. Seleman Jafo amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kwa usimamizi mzuri wa Sheria ya Mazingira katika mradi wa kufua umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP).

Pongezi hizo zimekuja mara baada ya Waziri huyo kuzuru eneo la mradi kwa lengo la kujiridhisha na hatua za ujenzi zilipofikia sambamba na suala la utunzaji na uhifadhi wa Mazingira katika eneo hilo.

" Mradi huu ni mkubwa wenye shughuli kubwa na nyingi zinazozalisha taka za kila aina na idadi ya watu takribani 12,000, hutegemei kukuta mazingira nadhifu kama haya, hizi zote ni juhudi za Baraza la Mazingira ambalo lilipiga kambi kabisa hapa kuhakikisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inasimamiwa hasa ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, Hongereni sana " Amesema Mhe. Jafo

Aidha Mhe. Jafo amesisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji ya mto kilombero na Ruaha na kuzitaja faida za mradi huu wa kufua umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere kuwa ni upatikanaji wa umeme wa uhakika, udhibiti wa mafuriko, uanzishwaji wa kilimo cha maji, kupunguza nishati ya kuni na mkaa na kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa Nchi yetu.

Nyingine ni ongezeko la mapato kwa Serikali, upatikanaji wa maji, kuanzisha utalii wa maji kwa njia ya boti pamoja na kutunza ikolojia ya hifadhi ya mbuga ya selou.