SHERIA YA MAZINGIRA IKO WAZI JUU YA UJENZI KWENYE VYANZO VYA MAJI -Dkt. GWAMAKA


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka ameitaka jamii kuheshimu sheria ya mazingira hasa kufanya ujenzi ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji, kwani maeneo ya mito na mabonde kisheria ni maeneo yanayo milikiwa na bonde la maji ambao wao wanawajibika kuhakikisha ustawi wa mazingira katika maeneo hayo.

Dkt. Gwamaka ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo hii, amesema kuwa sasa hivi kumetokea tatizo la wananchi kujenga ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji ambayo kisheria ni makosa makubwa. Hata hivyo ujenzi wa ndani ya mita sitini husababisha athari kubwa sana kwa wananchi wenyewe na kimazingira.

“kutokana na athari kubwa zinazojitokeza sisi kama Taasisi tunaendelea kuelimisha jamii kuwa kujenga ndani ya mita sitini unajiweka katika eneo hatarishi kwa mafuriko. Mbali na hayo mafuriko kama sasa hivi kumekuwa na tatizo la watu kutupa taka ndani ya mito, hivyo utakuwa sehemu ya dampo na hata ustawi wa mazingira unaharibika kwa ujumla wake”

Ameendelea kusisitiza kuwa ustawi wa mazingira una haribika kwa mfano katika maeneo ya bahari tunaustawi mkubwa sana wa mikoko ambayo ni hazina ya Taifa ambayo hutakiwi kuikata kwa sheria ya misitu kwa maana hiyo katika maeneo kama hayo hutakiwi kujenga wala kuendeleza kitu chochote

“Sisi kama Baraza tunachukua hatua hasa tunapogundua mwananchi amejenga ndani ya maeneo ya mikoko na kunabaadhi wameshitakiwa ambao wamejenga ndani ya mikoko lakini kubwa zaidi ni kuelimisha wananchi, sehemu kubwa ya wananchi hawaelewi hizi sheria sasa Baraza lipokwenye mkakati wa kuhakikisha kwamba kupitia vyombo vya habari na machapisho mbalimbali tunatoa elimu kwa jamii”

Dkt. Gwamaka pia amezungumzia namna bora ya ukusanyaji na utupaji wa taka zinazozalishwa majumbani, ameitaka Halimashauri na Kata zote nchini kuweka utaratibu unaofaa katika ukusanyaji wa taka, kwani kumekuwa na utaratibu usiofaa wa ukusanyaji taka ambao taka zinazozalisha zote kuwekwa pamoja bila kutenganishwa na kusababisha kazi kubwa kwenye madampo.

“Naisifu Halmashauri ya Mbeya wameshaanza kufanya tafiti na wametuhusisha, kwamba muda sio mrefu watatangaza taratibu gani ambao wakazi wa Mbeya watakuwa wanazitenga taka pale zinapozalishwa”

Hata hivyo Dkt.Gwamaka amesema kuwa kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuchambua taka kwani kuna taka kama karatasi, chuma na chupa za plastiki zinaleta fursa kwa wananchi kujipatia kipato na viwanda vyetu kuendeleza uzalishaji wake.

“Kama wananchi wataweka mazoea ya kutenganisha taka watakuwa wamepata fursa ya kujipatia kipato kutokana na taka hizo kunaviwanda vinahitaji taka kurejeleza lakini pia tutapunguza takataka katika madampo yetu”

Aidha Dkt. Gwamaka amesema kuwa kutenganishwa kwa taka zinaleta uchumi wa ndani kukua kwa maana kuwa viwanda ambavyo haviwezi kuagiza malighafi kutoka nchi za nje zinaweza kupata malighafi hapa hapa nchi hasa kwa upande wa vyuma chakavu na chupa za plastiki.