NEMC YAKUTANA NA MAKAMU WA RAIS MHE. BALOZI DKT. EMMANUEL JOHN NCHIMBI DODOMA


Ni katika kikao kazi cha kupitishana kwenye majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwenye kikaokazi cha kwanza na watendaji wake tangu kuteuliwa kwake chenye lengo la kupitishana kwenye majukumu ya utekelezaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma kilihusisha Menejimenti na watumishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Menejimenti ya Baraza pamoja na watendaji kutoka kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa masuala ya Carbon.

Akizungumza katika kikao hicho Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi amesema ni kikao cha kukumbushana wajibu tulionao kwa watanzania wa kudumisha Muungano pamoja na kusimamia masuala mazima ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini hasa ikizingatiwa dira ya maendeleo ya 2050 kipengele cha tatu kimezingatia masuala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na Ustahimilivu wa masuala mazima ya mabadiliko ya Tabianchi.

" Dhamana tuliyopewa ni kubwa, masuala ya Muungano, kutunza mazingira na uchumi wa buluu si vitu vya mchezo, ni lazima tumsaidie Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku miamoja (100) kutekeleza maagizo yahusuyo Muungano na Mazingira, tunao wajibu wa kuhakikisha Mazingira yanasimamiwa na kuhifadhiwa" Amesema Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Ametoa maagizo yafuatayo: kila mtumishi aisome ilani ya chama kilichopo madarakani pamoja na dira ya maendeleo ya 2050 kwani ndio msingi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali, masuala ya Muungano na Mazingira, Uchumi wa buluu, Carbon trade na nishati safi yasimamiwe na kutekelezwa kwa weledi, malengo yote ya utekelezaji wa shughuli za Muungano na Mazingira yawe na namna sahihi ya ufuatiliaji na utekelezaji wake ili kufikia azma iliyokubaliwa.

Maagizo mengine ni kuandaa mkakati wa mawasiliano utakaotoa muongozo wa namna ya kutangaza shughuli za mazingira, kuzingatia haki na stahiki za watumishi, kuhakikisha vijana wanaelewa maana halisi ya Muungano na kuuenzi pamoja na wakuu wa Taasisi kusimamia Sheria na miongozo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema NEMC inahitaji kupewa meno kwani kero za Mazingira zimekuwa nyingi hasa uchafuzi wa vyanzo vya maji na kelele chafuzi za Mazingira.

" Hakuna kitu kinanikera kama pale ocean road kila nikipita napakuta pachafu, panatoa harufu, matakataka yamezagaa, nikiwauliza NEMC.wanasema hawana meno" Mhe. Mhandisi Hamad Masauni.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja alipozungumza aliahidi kuyasimama na kuyatekeleza maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa kwa kushirikiana na watendaji wa Taasisi zote zilizo chini ya ofisi ya Makamu wa Rais.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Katibu Mkuu Mazingira Profesa Peter Msoffe na Naibu Katibu Mkuu Muungano Bw. Abdallah H. Mitawi.