WITO WATOLEWA KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KUACHA MATUMIZI YA KEMIKALI YA ZEBAKI (MERCURY)


Wito watolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini kuacha matumizi ya kemikali ya zebaki (Mercury) na kutumia teknolojia mbadala kwenye uchenjuaji wa dhahabu ili kulinda afya ya binadamu na Mazingira.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi. Cyprian Luhemeja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua Mkutano wa Kikanda wa Nchi za Afrika zinazotekeleza Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu (EHPMP), Mkutano unafanyika katika Hoteli ya Hyatti Regency jijini Dar es salaam.

Mhandisi Luhemeja amesema Mkutano huo umelenga majadiliano ya namna bora ya kuacha matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo, huku akitaja tani zaidi ya elfu 18 ya kemikali ya zebaki hutumika nchini Tanzania kwa mwaka hali inayohatarisha afya ya Viumbe hai na Mazingira.

“Lengo kuu la Kongamano hili ni kujadili namna bora ya kuondokana na matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo kwa sababu zebaki ni hatari kwa afya ya binadamu na Mazingira. Inakadiliwa kwa mwaka tunatumia kemikali ya zebaki zaidi ya tani elfu 18 ambapo sehemu kubwa ya watumiaji ni wachimbaji wadogo hivyo tunafanya juhudi ili kudhibiti matumizi ya kemikali ya zebaki” amesema Mhandisi. Cyprian Luhemeja

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema zebaki ni hatari kwa afya ya binadamu, vyanzo vya maji na mifumo mingine ya ikolojia, hivyo ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu kutumia teknolojia mbadala za kisasa kwa ajili ya uchenjuaji wa dhahabu.

Mkutano huo unakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali dunia zikiwemo nchi 5 zinazotekeleza Mradi huo ambazo ni Ghana, Kenya, Senegal, Zambia na Tanzania ambapo pia ni Nchi mwenyeji wa Mkutano.