WITO WATOLEWA KWA TAASISI ZA SERIKALI KUZINGATIA UFANYAJI WA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA KABLA YA MRADI KUANZA
Wito umetolewa kwa Taasisi za Serikali na binafsi kote Nchini kuzingatia umuhimu wa ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya mradi kuanza ili kuhifadhi Mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na jamii NEMC Bi. Lilian Lukambuzi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi cheti cha Tathmini hiyo kwa mratibu wa mradi wa kudhibiti matumizi ya Kemikali ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu kufuatia ujenzi wa kituo cha kutoa elimu ya udhibiti wa matumizi ya Zebaki kinachotarajiwa kujengwa Mkoani Geita.
Bi. Lukambuzi amesema ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) ndio msingi pekee utakaotoa nafasi ya kutambua athari za kimazingira katika eneo husika na kukupa nafasi ya kuendeleza mradi wowote huku ukizingatia udhibiti wa mazingira.
" Sisi kama NEMC ndio waratibu wa mradi wa kudhibiti matumizi ya kemikali ya zebaki hivyo ni lazima tuwe mstari wa mbele kutekeleza masuala ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake hasa ya ufanyaji wa Tathmnini ya Athari za Mazingira kwenye utekelezaji wa miradi kabla ya kuanza ili kutunza Mazingira'' alisema bi Lukambuzi.
Naye mratibu wa mradi wa kudhibiti matumizi ya kemikali ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia Mhandisi. Dkt. Befrina Igulu amesema mradi huo unatekelezwa katika Mikoa saba ya Geita, Shinyanga, Mara, Singida, Mwanza, Mbeya na Songwe hivyo ni muhimu kuwa na kituo kwa ajili ya mafunzo.
Ameongeza kuwa kituo hicho kimezingatia matakwa yote ya Kimazingira na kimekidhi vigezo vya Tathmnini ya Athari kwa Mazingira na kitakuwa na miundombinu wezeshi ya utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Amefafanua kuwa elimu ya matumizi salama ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu inatakiwa kizingatiwa hivyo kwa uwepo wa kituo hicho kutasaidia wachimbaji kwa makundi kupatiwa elimu ya matumizi salama ya zebaki
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15