WAZIRI JAFO ATOA NENO KATIKA HAFLA YA KUWAAGA WASTAAFU NEMC
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amemshukuru Dkt. Samuel Gwamaka Mafwenga kwa kuwa msaada mkubwa katika kufanikisha majukumu yake kama Wiziri mwenye dhamana ya Mazingira.
Waziri Jafo ameyasema hayo Aprili 27,2024 hoteli ya Serena alipokuwa akihutubia umma wa Wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika hafla ya kuwaaga wastaafu ambao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Samuel Gwamaka Mafwenga, aliyekuwa Meneja wa Kanda ya Kaskazini Bw. Lewis Nzali na Bw. Anold Kisiraga.
Waziri Jafo amesema kuwa alipoingia kwenye Wizara hiyo hakuwa anafahamu mengi kuhusu mazingira lakini kutokana na uwepo wa Dkt. Gwamaka aliweza kutekeleza majukumu yake kwa urahisi.
"Nilikuja Ofisi ya Makamu wa Rais nikiwa sijui mengi kuhusiana na Mazingira lakini ninyi kwa umoja wenu mkiongozwa na Dkt. Gwamaka mmenitengeneza nimeweza kuyajua Mazingira japo sio kwa asilimia zote lakini Kwa kiwango cha kuridhisha nimeweza kujua masuala ya Mazingira." Amesema Waziri Jafo.
Waziri Jafo ameongeza kwa kusema kuwa wakati anaanza kuitumikia Wizara yenye dhamana ya Mazingira alikuta Dkt. Gwamaka alimaliza muda wake lakini alimuombea ili aweze kuendelea na kazi ambapo ombi hilo lilikubaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Gwamaka akaongezewa muda wa kuendelea kulitumikia Baraza.
Akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Cyprian Luhemeja, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme amewapongeza wastaafu hao na kusifu utendaji kazi wa Dkt. Gwamaka.
"Kwakweli tunaufurahia, tunauenzi, tunauamini na tunauthamini utendaji wako na umeacha alama kwenye Baraza na hata hii mifuko ya plastiki tulijiuliza kama tutaweza lakini tuliweza kwa sababu ulitoka na ukasema." Amesema Bi. Christina.
Akitoa neno kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NEMC Mhandisi Profesa Esnat Chaggu amesema wakati wanaanza kutekeleza Majukumu yao walikuta malalamiko mengi sana lakini kwa kushirikiana na Dkt. Samuel Gwamaka waliweza kuyapunguza Kwa kiasi kikubwa.
"Tunashukuru kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkuu tuliweza kupunguza malalamiko Kwa kiasi kikubwa kwani alijitahidi na kupambana kurekebisha ofisini na mtaani kila mahali kuhakikisha kwamba malalamiko yanapungua, naishukuru pia Bodi ya Wakurugenzi NEMC kwani walikuwa tayari muda wote kumpa ushirikiano usiku na mchana." Amesema Profesa Chaggu.
Kwa upande wake Dkt. Gwamaka amewashukuru Wafanyakazi wa Baraza na amewaomba kumpatia ushirikiano Mkurugenzi Mkuu mpya wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi kama ambavyo wamempatia yeye kipindi akitekeleza Majukumu yake kama Mkurugenzi Mkuu wa Baraza.
Aidha amewatia moyo wafanyakazi hao wa Baraza kwani kazi wanayoifanya ni njema sana licha ya kuwa ni ngumu na wakati mwingi hata kuhatarisha maisha yao wakiwa katika kutekeleza Majukumu yao.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15