WAZIRI JAFO AFANYA ZIARA KIWANDA CHA RUIDA NA WATERCOM KUKAGUA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO ALIYOTOA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo amefanya ziara katika kiwanda cha Ruida Tanzania Company kilichopo Kisarawe II Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam kinachozalisha mabomba ya plastiki ya maji. Lengo la ziara hiyo ni kukagua mfumo wa maji taka ambao ulikua ni tatizo lilolalamikiwa na wananchi kipindi cha nyuma.
Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa kiwanda hiki mwanzo kilikuwa na changamoto kubwa sana na kilikuwa kinalalamikiwa na wananchi kutokana na maji machafu ambayo yanayotoka kiwandani na kuingia kwenye makazi yao. Ameendelea kusema kuwa alipofanya ziara kukagua kiwanda hicho alibaini changamoto hizo ambazo zilikuwa zinalalamikiwa na wananchi
“Nilipokuja hapa nilikuta hali ni mbaya nilitoa miezi mitatu kubadilisha mfumo wa uchujaji wa maji taka kwa kujenga chemba ambazo maji taka yaweze kusafishwa alikadhalika kununua mtambo wa kusafishia maji taka na maji hayo kutumika kwa matumizi mengine kiwandani. Leo hii nimekuja kukagua Kiwanda hiki cha Ruida kama kimetekeleza maagizo niliyotoa na ni kweli wametekeleza maagizo yote niliyotoa na nimefurahishwa sana” Mhe. Dkt. Jafo
Ameendelea kusema kuwa maji yanayotoka hapa sasa ni safi na salama kwa hiyo hata malalamiko kutoka kwa wananchi wetu waliokuwa wanalalamikia kiwanda hiki nadhani sasa yamekwisha. Amesema kuwa kiwanda hiki kimetekeleza kwa maagizo aliyowapa Kwa asilimia mia Moja. Vilevile amekitaka Kiwanda kilicho jirani kutekeleza maagizo aliyotoa ambayo wao walipewa miezi sita muda utakapofika atakagua kiwanda hicho kuona kama wametekeleza maagizo.
“Nasubiria miezi sita ifike kama agizo langu itakapokamilika nitaenda kutembelea kiwanda hicho cha mataili kilichopo karibu na kiwanda hiki na wakishindwa kutekeleza kiwanda hicho tutakifunga kwa sababu kitaendelea kuathiri maisha ya watu. Eneo hili lina viwanda vingi hivyo nawaagiza Maafisa mazingira wetu waliyokuwepo eneo hili wafuatilie viwanda hivyo inawezekana vinachafua mazingira kwa namna moja au nyingine” Mhe. Dkt. Jafo
Waziri Jafo pia alitembelea kiwanda cha Watercom Tanzania Limited kilichopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam kinachozalisha maji ya Afya. Mhe Jafo amesema kuwa lengo la kukagua kiwanda hicho ni kuona utekelezaji wa agizo alilotoa la kupiga marufuku karatasi laini zilizokuwa zinawekwa juu ya vifuniko vya chupa za maji. Amefurahishwa na kiwanda hicho kuchukua hatua ya kuacha mara moja kuweka karatasi hizo, lakini pia amepongeza kampuni nyingine ambazo zimechukua hatua ya utekelezaji wa agizo hilo
“Tulitoa miezi sita kampuni zote zinazozalisha karatasi laini katika vifuniko za chupa za maji kuacha kuzalisha karatasi hizo. Nashukuru sana wadau mbalimbali ndani ya Tanzania wameweza kutekeleza agizo hili kwa haraka sana leo hii nipo kiwanda cha maji cha Afya ambacho kipo Kigamboni kwa kweli nimefarijika sana nimeona agizo limetekelezwa vizuri sana. Pia niwashukuru makampuni mengine ambayo yametekeleza agizo hilo ikiwemo Kampuni ya Azam, Canadian, Jambo na makampuni mengine.” Mhe. Dkt. Jafo
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15