WAWEKEZAJI WA MIGODI NCHINI, TUNZENI MAZINGIRA KWA KUREJESHA MAENEO BAADA YA UCHIMBAJI MADINI - WAZIRI JAFO.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wawekezaji wa migodi kote nchini kuhakikisha wanarejesha maeneo waliofanyia shughuli za uchimbaji madini ili kuendelea kuyatunza na kuhifadhi mazingira ya maeneo husika kwa kuimarisha ikolojia yake kwa mstakabli mpana wa maendeleo endelevu ya Tanzania.
Ametoa maagizo hayo alipofanya ziara ya kutembelea maeneo ya uchimbaji wa madini na uwekezaji katika upande wa Makaa ya Mawe Mkoani Ruvuma kwa lengo la kujiridhisha na hali ya kimazingira katika maeneo hayo.
Amesema Serikali ya Tanzania iko mstari wa mbele katika kuvutia wawekezaji hasa wachimbaji wa madini kwa misingi ya Sheria na Kanuni za uwekezaji katika Nchi kwani ndio msingi wa maendeleo endelevu katika kukuza ajira na uchumi wa Nchi yetu, lakini haimaanishi kwamba itaacha kusimamia maeneo hayo na kuwataka wawekezaji wote kuzingatia miongozo katika kutekeleza shughuli zao.
‘Natoa maelekezo, kwako Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), suala la mazingira liko kwako kisheria , hivyo niwajibu wako kuhakikisha unatembelea migodi hii, hasa hii iliyopo Kanda ya Ziwa, jiridhishe na shughuli zao kama wanazingatia matwaka ya Sheria na maelekezo waliyopewa, na uhakikishe unatoa maelekezo ya haraka ili migodi hiyo ifanye urejeshaji wa ardhi iliyoharibiwa’ Amesema Dkt. Jafo
Kadhalika ameelekeza wawekezaji katika migodi hiyo kuhakikisha wanadhibiti utiririkaji wa maji ambayo inawezekana yakawa na athari kwa maisha ya watu kutokana na tindikali inayozalishwa pamoja na Salfa ambayo inaambatana na uchimbaji wa Makaa ya Mawe
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka alipokuwa akifafanua amesema atahakikisha anashirikiana bega kwa bega na sekta zote za uchimbaji wa rasilimali za migodi katika kuhakikisha utunzaji wa mazingira kwenye maeneo hayo unazingatiwa na kuwataka wawekezaji wote wa migodi kuandaa mipango ya Ukarabati wa Mazingira na kuwasilisha NEMC.
"Katika ziara tulioifanya, sehemu kubwa ya masharti ya vyeti vya mazingira yanafuatwa karibu kampuni zote tulizotembelea, hilo linatia moyo lakini bado kuna maeneo machache ambayo tunapenda waendelee kuyafanyia kazi kubwa". Amesema Dkt. Gwamaka
Kwa upande wa Wasimamizi wa Mazingira kwenye migodi hiyo,wameahidi kuyashughulikia maelekezo yote yaliyotolewa na kuhakikisha wanatunza mazingira katika zoezi la uchimbaji wa Makaa ya Mawe.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15